Kimataifa

AU yaondoa marufuku dhidi ya serikali ya Mali

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

BAMAKO, Mali

UMOJA wa Afrika (AU) umerejesha Mali miongoni mwa mataifa wanachama wake baada ya kuisimamisha kwa muda kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo mnamo Agosti 2020.

Uamuzi huo uliotangazwa Ijumaa jioni unajiri siku tatu baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kutangaza kuwa imeondoa vikwazo ilivyoiwekea nchi hiyo, ikisema inaunga mkono kurejeshwa kwa utawala wa Mali mikononi mwa raia.

Vikwazo hivyo vilijumuisha kufungwa kwa mipaka ya Mali na kupigwa marufuku kwa biashara kati ya nchi hiyo na mataifa ya ukanda huo. Hata hivyo, biashara ya bidhaa za kimsingi, dawa, vifaa vya kupambana na Covid-19 au umeme.

“Baraza la Amani na Usalama, kwa kuzingatia mabadiliko mazuri ya kisiasa na utawala, limeamua kuondoa hatua ya kusimamishwa kwa Mali kama mwanachama wa AU,” likasema baraza hilo katika ujumbe kupitia twitter.

Umoja wa Afrika wenye wanachama 55 ulitaja mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Ibrahim Boubacar Keita na kuitaja hatua hiyo kama “inayokiuka Katiba”.

Wanajeshi walifanya mapinduzi hayo baada ya Mali kuzongwa na maandamano ya raia wakiilaumu serikali kwa kushindwa kudhibiti visa vya mashambulio ya kigaidi na kuzorota kwa uchumi.

Japo hakuna maafa yaliyoshuhudiwa katika mapinduzi hayo, mataifa jirani ya Mali yalielezea kukerwa na hatua hiyo. Hii ni kwa sababu mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini humo mnamo 2012 yalifuatiwa na kuchipuza kwa mapigano kaskazini mwa Mali ambapo maelfu ya raia waliuawa. Mapigano hayo yalisababisha visa vya utovu wa usalama katika mataifa jirani ya Niger na Burkina Faso.

Mapinduzi ya kijeshi ya mwaka huu yalijiri baada ya wananchi kulalamikia kukithiri kwa mashambulio ya kigaidi kaskazini mwa Mali, mapigano ya kikabila na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na kuzorota kwa uchumi.

Kutokana na presha iliyotokana na vikwazo vikali vya Ecowas, kiongozi wa kijeshi wa Mali alitia saini makubaliano ya kurejesheshwa kwa utawala wa kiraia ndani ya miezi 18. Vile vile, aliteua kamati ambayo ilimteua Kanali Bah Ndaw, 70, kuwa kaimu Rais.

Mnamo Jumatatu Ndaw aliteua serikali ikiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni, Moctar Ouane, kama Waziri Mkuu. Baadhi ya wanajeshi wamepewa nyadhifa kuu katika serikali hiyo.

Nyadhifa za uwaziri kama vile Ulinzi, Usalama wa Ndani, Mipaka na Uwiano zimewaendea makanali wa jeshi.

Lakini raia pia waliteuliwa, akiwemo aliyekuwa mwendesha mashtaka Mohamed Sidda Dicko-Waziri wa Haki na aliyekuwa balozi Zeini Moulaye-Waziri wa Masuala ya Kigeni.