Kimataifa

AU yazindua mfumo wa dijitali kukomesha corona barani

August 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA FAUSTINE NGILA

HUKU mataifa kadha ya Afrika yekirejelea safari za ndege za kimataifa mwezi huu kwa mara ya kwanza tangu Machi, Umoja wa Afrika (AU)umezindua teknolojia ya kuhakikisha hakuna mlipuko wa maambukizi zaidi ya Covid-19.

Ili kuwapa imani abiria wa ndege kuhusu usalama wa kiafya wanapozuru mataifa ya kigeni, shirika hilo limeshirikiana na sekta ya kibinafsi kuunda jukwaa la kidijitali la kufuatilia watu waliotangamana na wagonjwa wa virusi vya corona.

Mradi huo kwa jina PanaBIOS, tayari unatumika nchini Ghana kuzuia kukusanyika kwa watu huku pia ukiwezesha safari za mipakani ambapo unawapa wasafiri vyeti vya kuthitbitisha hawana virusi hivyo.

Kulingana na Mshauri wa Rais kuhusu Masuala ya Afya nchinii Ghana Dkt Anthony Nsiah-Asare, serikali ya nchi hiyo ilianza kutumia uvumbuzi huo hapo Juni na umesaidia kwa maamuzi ya kufugua uchumi.

“Serikali iliamua kufanyia vipimo watu waliokisiwa kuwa wameambukizwa. Tulianza na shule na makanisa kwa kuwa ilikuwa lazima tufungue uchumi na tulihitaji mfumo wa kidijitali ambapo tungeweka data na kuona taarifa za virusi hivi kwa mbashara kwenye viwanja vya ndege na mipkani,” alisema kwenye mahojiano.

Teknolojia hiyo ina uwezo wa kufuatilia watu katika mikusanyiko, waliosafiri katika mataifa mengine na hivyo kutoa ramani kuhusu jinsi virusi hivyo vinasamaa.

“Nina imani kuwa kila taifa hapa barani litapendezwa na teknolojia hii kwa kuwa hakuna anayetaka kulipuka kwa virusi hivi tena. Visa vyote hapa Africa vilitoka mabara mengine, na iwapo hatutachukua hatua, kufunguliwa kwa uchumi huenda kukaongezea kusambaa kwa Covid-19 hapa barani kutoka mabara hayo tena,” alisema Dkt Nsiah-Asare.

PanaBIOS huwaarifu watu ambao wamekuwa kwa hatari ya kuambukizwa virusi hivyo na kuwashauri wapimwe. Watumizi wanaweza kuona matokeo yao na kupewa vyeti vya kuwaruhusu kupita mipakani. Ni teknolojia isiyo na malipo na inaweza kutumika mataifa yote 55 ya Afrika.

Hata hivyo, kulingana na mlumbi wa sera za Afrika Prof PLO Lumbumba, Kenya itahitaji kuielewa teknolojia hiyo kwanza kabla ya kufikiria kuitumia.

“Tunahitaji kuielewa mwanzo na kung’amua inavyoendeshwa,” aliambia Taifa Leo.

Lakini mwanasayansi wa data humu nchini Timothy Oriedo, amesema teknolojia hiyo itasaidia pakubwa kudhibiti kuongezeka kwa ugonjwa huo.

“Kufuatiliwa kwa wanaotangama na wagonjwa wa corona kutasaidia serikali kubadilisha mwenendo wa Wakenya ambao bado wanakusanyika kwa vikundi. Kuwatumia arafa ya simu kwamba wametangama na mtu anayeugua corona kutabadilisha tabia yake na hivyo kusalia nyumbani,” alisema mtaalamu huyo.

Hata hivyo, Bw Orideo aliyashauri mashirika yanayohusika kwa mradi huo kulinda data ya wagonjwa na watu wanaofuatiliwa.

“Iwapo serikali ya Kenya itaamua kutumia mfumo huo, basi wanaohusika wanafaa kufuata Sheria ya Kulinda Data kwa kuwaomba wagonnjwa kibali cha kutumia data yao na pia kuhakikisha haitauzwa kwa manufaa ya kibiashara,”