Balozi wa Amerika nchini Kenya Meg Whitman ambaye amejiuzulu wadhifa wake kutokana na shinikizo kutoka kwa Wakenya. Picha|Maktaba
Balozi wa Amerika nchini Kenya Meg Whitman amejiuzulu.
Bi Whitman aliwasilisha barua yake kwa Rais Joe Biden na kutangazia wafanyakazi wa ubalozi huo hatua yake Jumatano, Novemba 13, 2024 asubuhi.
“Leo, nilitangaza kwa timu yangu katika ubalozi wa Amerika kwamba niliwasilisha barua yangu ya kujiuzulu kwa Rais Biden. Imekuwa heshima na fursa kubwa kuwahudumia watu wa Amerika kupitia kuimarisha ushirikiano wetu na Kenya,” Bi Whitman alisema.
Hatua yake inajiri baada ya Wakenya kumtaka Rais Mteule wa Amerika Donald Trump kumuondoa Kenya akisema amesaidia Serikali ya Rais William Ruto ‘kukandamiza’ raia.
“Ninajivunia kuongoza ajenda inayozingatia watu kuokoa maisha, kuongeza usalama, na kuunda fursa za kiuchumi kwa Wakenya na Waamareka. Kutoka kwa utoaji wa ufadhili wa dharura kupunguza athari za mafuriko makubwa mwaka wa 2023 hadi mapambano yanayoendelea dhidi ya malaria, Ukimwi, na MPOX, serikali ya Amerika inatanguliza afya na ustawi wa marafiki wetu nchini Kenya,” alisema Bi Whitman.
Akitangaza ufanisi wake Kenya, alisema wakati wa muhula wake Kenya iliibuka kuwa mshirika mkuu wa kwanza asiye wa NATO katika kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, na hivyo kuonyesha “umuhimu ambao nchi zetu zinaweka kulinda maadili yetu ya pamoja ya kidemokrasia na kuimarisha usalama.”
Aliongeza: “Juhudi zangu pia zilifungua milango kwa kampuni zaidi za Amerika kufanya biashara nchini Kenya.”
Bi Whitman aliteuliwa balozi wa Amerika nchini Kenya mwaka wa 2022 na Wakenya wengi wanahisi alisaidia serikali ya Kenya Kwanza kuingia mamlakani.
“Nilipofika 2022, nililenga kupanua uhusiano huu wa Kenya na Amerika. Pia tuliitikia mahitaji makubwa ya huduma zetu za kibalozi, na hivyo kupunguza muda wa kusubiri kupata viza vya watu wasio wahamiaji kutoka zaidi ya miaka miwili hadi takriban miezi miwili miongoni mwa huduma zingine tulizoboresha,” alisema.
“Kama mabalozi wote wa Amerika, ninahudumu kwa hisani ya Rais. Watu wa Amerika wamezungumza, na Rais mpya ataapishwa Januari. Namtakia mafanikio yeye na timu yake mpya. Ubalozi wetu unanufaika na wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu wa Kenya na Amerika,” alisema,
“Sina shaka kwamba ushirikiano wetu wa miaka 60 utaendelea kuimarika na kuwahudumia Wamareka na Wakenya.”
“Tunapolenga kujenga mataifa yenye ustawi, afya, usalama na demokrasia zaidi, mahusiano yetu yana nguvu zaidi kuliko hapo awali, na nina hakika mwelekeo huu utaendelea. Nitaondoka Kenya nikiwa nimejawa na shukrani kwa timu ambayo imefanya kazi bila kuchoka,” alisema.
Hata hivyo, Wakenya walisherehekea kujizulu kwake wakisema amechelewa kuondoka Kenya.