Baraza la kijeshi Sudan ladai lilitibua njama ya mapinduzi
Na MASHIRIKA
BARAZA la kijeshi linalotawala Sudan, lilitibua jaribio la mapinduzi, jenerali wa cheo cha juu alitangaza kupitia runinga mnamo Alhamisi akisema maafisa 12 na wanajeshi wanne walikamatwa.
Tangazo hilo lilijiri siku chache baada ya baraza tawala la kijeshi na viongozi wa waandamanaji, kukubaliana kumaliza mzozo wa kisiasa uliofuatia kutimuliwa kwa Rais wa muda mrefu Omar al-Bashir.
“Maafisa na wanajeshi kutoka jeshi la nchi kavu na Huduma ya Taifa ya Ujasusi na Usalama, baadhi yao waliostaafu, walikuwa wakijaribu kutekeleza mapinduzi,” Jenerali Jamal Omar, wa baraza tawala la kijeshi alisema kwenye taarifa iliyopeperushwa moja kwa moja kwenye runinga.
“Vikosi vya usalama vilifaulu kutibua jaribio hilo,” alisema lakini hakueleza jaribio hilo lilitendeka lini.
Omar alisema kwamba maafisa 12 walikamatwa, watano wao wakiwa waliostaafu jeshini na kwamba vikosi vya usalama vinamsaka aliyepanga mapinduzi hayo.
“Hili ni jaribio la kuzuia makubaliano ambayo baraza tawala la mpito la kijeshi na Muungano wa Uhuru na Mageuzi waliafikiana kufungua barabara ya watu wa Sudan kutimiza matakwa yao,” alisema Omar.
Tangazo hilo lilijiri pia wakati ambao majenerali na viongozi wa waandamanaji walikuwa wakipiga msasa makubaliano yao katika hoteli moja ya kifahari jijini Khartoum.
Pande zote mbili zilifanya mazungumzo ya kina usiku kutwa na wakakubaliana kukutana tena Jumamosi, wapatanishi walieleza wanahabari.
Makubaliano hayo ya kihistoria yanayolenga kubuni baraza jipya la utawala la mpito yaliafikiwa wiki jana kufuatia juhudi za wapatanishi kutoka Muungano wa Afrika na wajumbe kutoka Ethiopia.
Mwanzo mzuri
Kubuniwa kwa baraza jipya la utawala ni hatua ya kwanza kuelekea kubuniwa kwa utawala wa kiraia Sudan walivyotaka waandamanaji.
Sudan imekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu maandamano yalipoanza Desemba 19, 2018, dhidi ya utawala wa Bashir.
Kufuatia maandamano hayo, jeshi lilimtimua Bashir mnamo Aprili 11 lakini majenerali waliotwaa mamlaka walikataa matakwa ya waandamanaji kukabidhi uongozi kwa serikali ya kiraia.
Taharuki ilitanda kati ya pande zote mbili baada ya vikosi vya usalama kuvamia waandamanaji waliokusanyika nje ya makao makuu ya jeshi jijini Khartoum na kuua watu zaidi ya 100.
Uvamizi huo ulijiri baada ya mazungumzo kati ya majenerali na viongozi wa waandamanaji kukwama Mei pande zote zilipokosa kuelewana kuhusu aliyepaswa kuongoza baraza la utawala.
Juhudi za upatanishi zilizoongozwa na Muungano wa Afrika na Ethiopia, zilizaa matunda Julai 5 na pande zote zikakubali kuunda baraza jipya la utawala kusimamia kipindi cha mpito cha miaka mitatu.