Kimataifa

Besigye, Bobi Wine katika kikao cha siri kuhusu 2021

October 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ERIASA MUKIIBI SSERUNJOGI, DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

IMEFICHUKA kwamba Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Dkt Kizza Besigye na Mwanamuziki Mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine wameanzisha mashauriano kisiri kuhusu watakavyoungana kwa nia ya kumshinda Rais Yoweri Museveni kwenye uchaguzi wa 2021.

Inadaiwa mazungumzo hayo yamekuwa yakiendelea kichinichini huku wawakilishi wa viongozi hao wawili wakipanga mikakati maridhawa ya kuhakikisha wanaungana na kumvua Rais Museveni mamlaka ya utawala mwaka huo wa uchaguzi.

Mnamo mwezi Mei, wanachama wa vuguvugu la ‘Serikali ya Wananchi’ linaloongozwa na Dkt Besigye na wenzao wa vuguvugu la ‘Mamlaka ya Wananchi’ linalosimamiwa na Kyagulanyi walitoa tangazo la wazi kwamba watashirikiana kwa lengo la kushinda uchaguzi wa mwaka wa 2021.

Aidha imebainika wawakilishi wa viongozi hao wawili wamekuwa wakiandaa mikutano baada ya tangazo hilo na wameanza kukubaliana kuhusu masuala ya kimsingi huku wakiwa na nia kuu ya kushinda Urais.

Duru zinaarifu kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wawili hao kuungana huku wawakilishi wa Kyagulanyi wakiwarai wenzao wanaomwakilisha Dkt Besigye kukubali na kuunga mkono mwanasiasa huyo chipukizi kwenye uchaguzi huo.

Vilevile imebainika kwamba kuna imani kutoka mrengo wa Kyagulanyi kwamba mwanasiasa huyo chipukizi ana uwezo mkubwa wa kumshinda Rais Museveni ikilinganishwa na Dkt Besigye ambaye ameibuka wa pili kila mara anapowania dhidi ya kiongozi huyo mkongwe.

Aidha inadaiwa kwamba wawakilishi wa Kyagulanyi wamelegeza msimamo na hata kufichua kwamba mwaniaji wao yupo tayari kuhama chama chake na kuwania Urais kwa tiketi ya chama cha FDC kinachoongozwa na Dkt Besigye, iwapo kigogo huyo wa siasa za upinzani atakubali kumuunga mkono.

Wawakilishi

Jopo la wawakilishi wa Dkt Besigye linaongozwa na mwanasiasa Wafula Oguttu ambaye wakati moja alikuwa mbunge, kiongozi wa upinzani bungeni na msemaji wa FDC.

Kyagulanyi naye mara ya kwanza alimteua mbunge wa Butambala, Muwanga Kivumbi kumwakilisha kwenye mazungumzo hayo lakini baadaye alimpiga kalamu kisha akamteua David Lubongoya kuchukua nafasi yake.

Kivumbi ni mwanachama wa chama cha DP na amejizolea sifa kama mwanaharakati ambaye amepinga utawala wa kimabavu wa Rais Museveni kwa miaka mingi.

Pia amekuwa mwanachama wa Vuguvugu la vijana wanaopigania demokrasia Uganda(UYD) tangu wakati alipokuwa mwanafunzi chuoni.

Hata hivyo, Oguttu na Lubongonya walikataa kufichua palipofikia mazungumzo hayo, wote wakisisitiza kwamba waliamrishwa kufanya kazi na kutofichua lolote kwa wanahabari.