Biya, 92, aahidi Gen Z wa Cameroon mazuri akishinda muhula wa nane
RAIS wa Cameroon, Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92 na anayeshikilia rekodi ya kiongozi wa nchi aliye hai mwenye umri mkubwa zaidi duniani, ameahidi wananchi wa taifa hilo kuwa “mazuri bado yanakuja” huku akigombea muhula wake wa nane mfululizo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumapili.
Tangu aingie madarakani mwaka 1982, Biya ameendelea kuongoza bila kukatizwa, na iwapo atashinda uchaguzi wa mwaka huu, ataendelea kuwa madarakani hadi atakapofikisha umri wa miaka 99. Hii itamaanisha kuwa atakuwa ameongoza Cameroon kwa kipindi cha karibu miaka 50.
Licha ya wito wa muda mrefu kutoka kwa wapinzani na raia wa kawaida kumtaka astaafu, Biya amepuuza shinikizo hizo. Katika kipindi cha kampeni, amekosolewa vikali kwa kutoshiriki kikamilifu katika mikutano ya hadhara. Alichagua kuhudhuria mkutano mmoja pekee wa kampeni, huku akitumia muda mwingi kwenye ziara za kibinafsi barani Ulaya.
Ili kukabiliana na ukosoaji wa kutumia video iliyotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI), Biya alirejea nchini kwa haraka na kuelekea kaskazini mwa Cameroon, katika mji wa Maroua eneo lenye wapiga kura wengi. Huko alihutubia maelfu ya wafuasi wa chama chake, akiwaahidi vijana na wanawake kuwa serikali yake itapatia kipaumbele mahitaji yao katika muhula unaofuata.
Alisisitiza kuwa atatekeleza ahadi zake, na kuwaomba wamwamini na kumpa kura zao tena.
Hata hivyo, wachambuzi wa kisiasa wanasema kwamba tangu Biya aingie madarakani, malengo yake makuu yamekuwa ni kudumu mamlakani, mara nyingi kwa gharama ya maendeleo ya wananchi. Dkt Immanuel Wanah anaeleza kuwa utawala wa Biya umekuwa ukilenga zaidi usalama wa kisiasa binafsi badala ya ustawi wa raia wa kawaida. Hii inachangiwa na jaribio la mapinduzi lililotibuliwa mwaka 1984, ambalo linaaminika kuwa lilimfanya awe makini mno kuhusu hatari za kupoteza madaraka.
Kwa sababu hiyo, zaidi ya asilimia 60 ya Wacameroon ambao ni vijana walio chini ya miaka 25 hawajawahi kumjua rais mwingine zaidi ya Biya.
Marie Flore Mboussi, mwanaharakati mchanga wa kisiasa, anaamini kuwa muda umefika kwa uongozi mpya na anasema kuwa “kudumu madarakani kwa muda mrefu kunazalisha aina fulani ya uvivu wa utawala.” Anasema kuwa baada ya miaka 43, wananchi wamechoka na wanataka mabadiliko.
Uchaguzi huu unafanyika katika mazingira yenye changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi: mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, huduma duni za afya na elimu, usalama duni katika baadhi ya maeneo, na shutuma za kuendelea kwa vitendo vya rushwa.
Changamoto ya ajira kwa vijana ni kubwa sana na imekuwa hoja kuu kwa wagombea wengi wa urais. Takwimu kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) zinaonyesha kuwa karibu asilimia 40 ya vijana wa Cameroon wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 hawana ajira. Aidha, asilimia 23 ya wahitimu wa vyuo vikuu wana tatizo la kupata ajira rasmi.
Vanina Nzekui, kijana mwenye umri wa miaka 26 aliyehitimu masomo ya juu, anasema vijana wengi wa Cameroon wana ndoto za kuondoka nchini kwa sababu wanahisi hawana nafasi ya kufanikiwa ndani ya nchi yao. Anasema kuwa wanaamini nafasi zote muhimu zimechukuliwa na viongozi wa zamani na hakuna njia ya kuingia katika mifumo rasmi ya ajira au uongozi. Hii, anasema, inazuia mchango wao kwa maendeleo ya taifa.
Hata hivyo, Aziseh Mbi, mwenye umri wa miaka 23, anasema umri wa mtu haupaswi kuwa kigezo pekee cha kumhukumu kiongozi. Kwa mtazamo wake, Rais Biya amefanikisha mambo kadhaa muhimu, hasa katika sekta za vijana, na hivyo hastahili kubezwa kwa sababu ya umri wake pekee.