Kimataifa

Buhari kukutana na Trump White House

April 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

RAIS wa Nigeria Muhammadu Buhari, Jumatatu atakutana na Rais Donald Trump wa Amerika jijini Washington na kuwa kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kukaribishwa na Trump katika ikulu ya White House.

Trump anapigwa darubini kufuatia tamko lake alilotukana nchi za Afrika ambalo alikanusha baadaye.

Uhusiano wa Trump na mataifa ya Afrika uliingia ndoa zaidi Machi mwaka huu alipomfuta kazi aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Rex Tillerson akiwa Nigeria kwenye ziara yake ya kwanza Afrika.

Hatua hiyo ilifichua machache kuhusu sera za utawala wa Trump kwa Afrika. Ziara ya Buhari inajiri siku chache baada ya Trump kukutana na Chansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Kulingana na taarifa ya ikulu ya White House, mazungumzo ya Buhari na Trump yatahusu vita dhidi ya ugaidi na ukosefu wa usalama, ukuaji wa uchumi na demokrasia nchini Nigeria ambayo itaandaa uchaguzi wa urais Februari mwaka ujao.

Nigeria inapigana na magaidi wa Boko Haram kwa mwaka wa tisa sasa na watu zaidi ya 20,000 wameuawa na magaidi hao.