COVID-19: Magufuli kutuma ndege Madagascar iwachukulie Watanzania 'dawa' aina ya chai ya mitishamba
MASHIRIKA na CHARLES WASONGA
RAIS wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema taifa lake litaagiza dawa ya kienyeji ambayo imedaiwa kutibu wagonjwa wa Covid-19 nchini Madagascar.
Lakini tofauti na viongozi wa mataifa jirani ya Uganda na Kenya, Dkt Magufuli ameshikilia kuwa kamwe hatatoa amri ya kudhibiti shughuli za kawaida katika miji mikuu nchini humo kama vile Dar es Salaam na Dodoma.
Vilevile, ametangaza kuwa siku chache zijazo ataruhusu kurejelewa kwa ligi kuu ya kandanda nchini humo akisema “imebainika wazi kuwa wanaspoti hawaambukizwi virusi vya corona.”
Na taifa la Congo-Brazzaville pia limeahidi kuagiza kinywaji hicho ambacho kimesifiwa na Rais wa Madagascar Andry Rajoelina kama tiba kamili ya ugonjwa huo. Japo ni jumla jumla ya watu 135 wameambukizwa virusi hivyo Madagascar hamna hata mmoja amefariki huko 80 wakipona.
Kufikia sasa ugonjwa huo umesababishwa vifo vya zaidi ya watu 230,000 kote ulimwenguni, Amerika ikiongozwa kwa kuandikisha zaidi ya vifo 66,000.
Dawa hii inayojulikana kama Covid-Organics (CVO) inatengenezwa kutokana na mmea unaojulikana kama Artemisia – chanzo cha viungo vinavyotumiwa kutengeneza dawa ya kutibu malaria.
Na huuzwa kwa hali ya majimaji ambayo hupakiwa katika chupa za kuanzia mililita 250 hadi lita moja.
Lakini Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeshikilia kuwa kufikia sasa hakuna tiba ya Covid-19 na likawashauri watu dhidi ya kutumia dawa zisizoidhinishwa.
“WHO haijaidhinisha matumizi ya dawa yoyote kwa ajili ya kuzuia au kutibu Covid-19,” shirika hilo likasema kwenye taarifa.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus alinukuliwa akisema kuwa “hakuna njia ya mkato katika juhudi za kusaka dawa ya kutibu Covid-19.”
Majaribio yanaendelea katika ngazi ya kimataifa katika juhudi za kutafuta dawa bora, WHO iliongeza.
Mnamo Machi 2020 Shirika la National Centre for Complementary and Integrative Health, lenye makao yake nchini Amerika lilionya dhidi ya matumizi ya dawa za kienyeji kutibu ugonjwa wa Covid-19. Lilishikilia kujwa njia bora ya kuzuia maambukizi ni kutojitenga na wale ambao tayari wameambukizwa.
Licha ya hayo kinywaji cha CVO kimeendelea kupata umaarufu katika mataifa mengine barani Afrika.
Mnamo Jumapili Madagascar iliwasilisha shehena ya dawa hiyo nchini Guinea-Bissau.
Rais Rajoelina pia alisema kuwa balozi maalum wa nchini hiyo nchini Equitorial Guinea aliwasilisha dawa hiyo katika taifa hilo lililoko magharibi mwa Afrika.
Nchini Tanzania, Rais Magufuli alitangaza kuwa tayari amekamilisha mazungunzo na serikali ya Madagascar na kwamba atatuma ndege huko kwenda kuchukua dawa hiyo.
“Nimezungumza na mwenzangu wa Madagascar ameniambia wamegundua dawa. Tutatuma ndege ilete dawa hiyo ili Watanzania nao wafaidi. Kama serikali, tunafanya kazi usiku na mchana,” akasema.
Rais Magufuli amekosolewa kwa kudinda kuchukua hatua kali dhidi ya janga la corona.
Ameendelea kuhimiza raia kutangamana katika maeneo ya ibada, ilhali mataifa mengi ulimwenguni yamepiga marufuku mikusanyiko kama hiyo kama hatua ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.
Kufikia sasa Tanzania imethibitisha zaidi ya visa 480 vya maambukizi.