Kimataifa

Demokrasia yayumba Afrika Mashariki Chadema ikizuiwa kushiriki uchaguzi Tanzania

Na REUTERS April 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DAR ES SALAM, Tanzania

CHAMA kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimezimwa kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba, afisa mmoja wa tume ya uchaguzi amesema.

Hatua hiyo ilichukuliwa siku chache baada ya kiongozi wa Chadema, Bw Tundu Lissu, kushtakiwa kwa kosa la uhaini kutokana na madai kuwa alijaribu kuvuruga uchaguzi huo.

Mkurugenzi wa masuala ya uchaguzi katika Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima, alisema Jumamosi jioni kuwa Chadema haikuidhinishwa kushiriki kura kwa sababu ilikosa kutia saini kanuni za nidhamu uchaguzini kufikia siku hiyo, na hivyo haiwezi kuruhusiwa kushiriki katika chaguzi za urais na ubunge baadaye mwaka huu.

“Chama chochote ambacho hakijatia saini kanuni ya nidhamu hakitaruhusiwa kushirika katika uchaguzi mkuu,” Bw Kailima alisema na kuongeza kuwa Chadema pia haitaruhusiwa kushiriki chaguzi zote ndogo hadi 2030.

Awali, Chadema ilikuwa imesema itasusia kura hiyo endapo mageuzi hayatafanywa kwa mfumo wa uchaguzi ambao inasema unapendelea chama tawala.

Bw Lissu, ambaye amewahi kuwa mgombea urais, alishtikiwa kwa uhaini siku ya Ijumaa.

Uamuzi wa kuzima chama chake kushiriki uchaguzi mkuu ujao utaathiri pakubwa rekodi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu udumishaji haki za binadamu katika harakati zake za kutaka achaguliwe tena kama Rais.

Watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa vyama vya upinzani wameisuta serikali ya Rais Samia kutokana na mienendo yake ya kudhulumu wapinzani wake wa kisiasa, wakitaja msururu wa visa vya utekaji nyara na mauaji ya wafuasi wa upinzani.

Serikali imekana madai hayo na kuanzisha uchunguzi kuhusu visa vya utekaji nyara.

Awali chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), kilishikilia kuwa serikali inaheshimu haki za binadamu na kukansa kuhusika katika visa vya ukiukaji wa haki hizo.

Chadema haijatoa kauli yoyote kuhusu uamuzi wa tume ya INEC kuizima kushiriki uchaguzi mkuu.

Mnamo Jumamosi, chama hicho kilisema hakingeshiri hafla ya kutia saini kanuni kuhusu udumishaji mienendo bora wakati wa uchaguzi. Kilidai hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zake kutaka mageuzi katika mfumo wa uchaguzi na uongozi.

Mnamo Alhamisi waendesha mashtaka walidai Bw Lissu alichochea umma kuanzisha maasi na kuvuruga maandalizi ya uchaguzi. Hakutakiwa kujibu mashtaka hayo ya uhaini, ambayo adhabu yake ni kunyongwa.