Kimataifa

Evariste Ndayishimiye ndiye rais mpya wa Burundi

May 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

Mgombea  urais wa chama tawala cha Burundi Bw Evariste Ndayishimiye ameshinda uchaguzi wa urais uliofanyika wiki iliyopita akiwa na asilimia 68.7 ya kura zote, Tume ya Uchaguzi ya Burundi imetangaza.

Jenerali huyo mstaafu wa jeshi atachukua hatamu za uongozi kutoka kwa Rais Pierre Nkurunziza baada ya kumshinda mwezake wa upizani Agwathon Rwasa aliyepata asilimia 24.19 ya kura. Waliopiga kura walikuwa watu zaidi ya milioni 4.

Bw Rwasa alisema kwamba kura hizo hazikuwa halali kwani baadhi ya wilaya zilikuwa zinarekodi kura nyingi kuliko wapigakura waliojiandikisha. Aliilaumu serikali kwa kuwazuia wanahabari kufuatilia uchaguzi siku ya kupiga kura huku akisema kwamba hiyo ilichangia wizi wa kura.

Kura hizo zilifikisha mwisho utawala wa Bw Nkurunziza ambaye alitawala kwa miaka 15, kuanzia mwaka wa 2005 hadi 2020 baada ya jaribio lake la kungombea urais mara ya tatu kufeli na kuleta vita na machafuko.

Kura hizo ziliendelea licha ya uwepo wa ugonjwa wa corona huku wawaniaji saba wakijitokeza.

Ndayishimiye anatarajiwa kuapishwa hapo Agosti mwaka huu.