Gen Z wa Uganda walivyonyamazishwa hata kabla waseme ‘ngwe’ barabarani
KAMPALA, UGANDA
VIKOSI vya usalama nchini Uganda viliwazuia vijana kadhaa jijini Kampala waliokuwa wakishiriki katika maandamano yaliyopigwa marufuku na serikali.
Waandamanaji hao walisema wajitokeza katika barabara za jiji hilo kupinga jambo walilolitaja kama mwenendo wa watawala wa nchi hiyo kutopambana na ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Wanahabari wa shirika la Reuters walishuhudia maafisa wa usalama wakiwakamata vijana hao.
Aidha, video moja iliyopakiwa katika akaunti ya X ya NTV Uganda ilionyesha kundi la vijana lilikabiliwa na kunaswa na polisi walipokuwa wakiandamana.
Waandamanaji hao walibeba mabango na kutoa kauli za kupinga ufisadi. Mmoja alivalia tishati yenye maneno “Speaker Must Resign” (Sharti Spika Ajiuzulu).
Msemaji wa polisi hakufichua idadi ya watu waliokamatwa na polisi na kuzuiliwa.
Serikali ya Uganda, kupitia Idara ya Polisi, ilipiga marufuku maandamano hayo, ikidai kuwa na habari za kijasusi kwamba vijana wahalifu walikuwa wanapanga kuingilia maandamano ili kupora na kuharibu mali ya umma na mali ya kibinafsi.
Maafisa wa Jeshi la Uganda na polisi walikuwa wameletwa kushika doria karibu na majengo ya bunge na maeneo kadhaa katikati mwa jiji la Kampala kwa lengo la kuwazuia waandamanaji hao.
Kuanzia usiku wa kuamkia jana, barabara zote za kuelekea majengo ya bunge zilikuwa zimefungwa.
Ni wabunge na wafanyakazi wa bunge pekee waliruhusiwa kupita katika barabara hizo.
Picha zilizopeperushwa na NTV Uganda zilionyesha magari ya wanajeshi yenye vifaa vya kukinga risasi yakizunguka maeneo ya karibu na bunge.
Wenye biashara mbalimbali karibu na majengo ya bunge walikuwa na wakati mgumu kuingia katika maduka na maeneo yao ya kibiashara.
“Maeneo haya yamegeuzwa Eneo uwanja wa vita,” akasema Edwin Mugisha, anayefanya kazi jijini Kampala, akirejesha magari ya kivita ya wanajeshi yaliyokuwa yakizunguka jijini Kampala.
Jumatatu, polisi walizingira afisi za chama kikuu cha upinzani nchini Uganda. Serikali ilidai kuwa chama hicho ndicho kilihusika katika maandalizi ya maandamano hayo ya kupinga serikali. Baadhi ya maafisa wa chama hicho walizuiliwa, wakiwemo wabunge wake.
Chama hicho, National Unity Platform (NUP) kilikana madai hayo kikiyataja kama ambayo “hayana msingi wowote”.
Kiongozi wa chama hicho Robert Kyagulanyi (maarufu kama Bobi Wine) alisema baadhi ya maafisa wake walidhulumiwa na maafisa hao wa usalama walipokuwa wakikamatwa.
“Waoga hawa wamegeuza makao makuu ya National Unity Platform kuwa kambi ya jeshi,” Bobi Wine akaandika katika mtandao wa X.
Viongozi wa upinzani na watetezi wa haki za kibinadamu wanadai kuwa visa vya uporaji na ubadhirifu wa pesa za serikali vimekithiri zaidi nchini Uganda.
Wamemkashifu Rais Yoweri Museveni kwa kufeli kuagiza kukamatwa na kushtakiwa kwa maafisa wakuu wa serikali yake wanaoshiriki maovu hao.