Kimataifa

Gharama ya juu ya maisha ilitikisa serikali nyingi 2024

Na BENSON MATHEKA December 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JAPO mfumuko wa bei ulishuka katika nchi nyingi ulimwenguni mwaka wa 2024,  wapiga kura hawakujali na kuelezea hasira zao uchaguzini

Wakiwa wamekasirishwa na kupanda kwa bei za kila kitu kuanzia mayai hadi kawi katika miaka michache iliyopita, waliadhibu vyama vilivyokuwa madarakani kila walipopata fursa. Zigo la mfumuko wa bei linaendelea, na vyama tawala vililaumiwa na kuadhibiwa katika uchaguzi baada ya uchaguzi.

Hasira za raia zilikuwa sawa katika nchi masikini na tajiri, zenye nguvu na zile zinazotegemea misaada.

Gharama ya juu ya maisha

Nchini Amerika, gharama ya juu ya maisha ilimsaidia Donald Trump kushinda muhula wa pili kama rais miaka minne baada kuondoka  Ikulu ya White House  kupitia uchaguzi ambao alidai ulikumbwa na udanganyifu.

Wafuasi wake walishindwa katika jitihada zao za kubatilisha kushindwa kwa Trump kwa kuvamia Bunge la Amerika  mnamo Januari 6, 2021.

Mwaka huu, walitoa sauti zao kwenye kura, wakikaribisha uongozi mpya  ambao unaweza kujaribu taasisi za kidemokrasia nyumbani na kuvuruga uhusiano wa Amerika na nchi nyingine ulimwenguni.

Hisia za kulalamikia mfumuko wa bei pia zilileta serikali mpya nchini Uingereza na Botswana, Ureno na Panama. Wapiga kura wa Korea Kusini waliweka upinzani madarakani katika bunge, kupiga darubini Rais Yoon Suk Yeol.

Mapema  Desemba, rais Yeol alitangaza sheria ya kijeshi, hatua ambayo Bunge ilibadilisha haraka. Uchaguzi pia ulitikisa Ufaransa, Ujerumani, Japan na India.

Putin achaguliwa tena kuwa rais

Nchini Urusi, mambo yalibaki ilivyokuwa uongozini, Vladimir Putin alichaguliwa tena kuwa rais kwa asilimia 88 ya kura, akiweka  rekodi katika Urusi baada ya kuvunjika kwa muungano wa Usovieti.

Moscow iliendelea  na vita vyake dhidi ya Ukraine. Swali kubwa ni athari ambazo kurejea kwa Trump katika Ikulu ya White House kutakuwa kwa mzozo huo.

Trump,  ameahidi kumaliza vita hivyo ndani ya siku moja. Wengi nchini Ukraine na kwingineko barani Ulaya wanahofia hilo linaweza kumaanisha kumuunga mkono Putin.

Katika Mashariki ya Kati, Israel iliendelea na vita vyake dhidi ya Gaza na kuzipanua hadi Lebanon, ambapo iliacha Hezbollah inayoungwa mkono na Iran ikiwa imeharibiwa na katika mkanganyiko. Nchini Syria, kundi lililoratibiwa vyema la waasi lilimpindua Bashar al-Assad na sasa linataka kuongoza nchi.

Katika biashara, kampuni duniani kote zilipambana kukumbatia ujio wa Akili Unde.