Hali ya wasiwasi yaongezeka Cameroon, serikali ikiwakamata waandamanaji kadhaa
SERIKALI ya Cameroon imewakamata waandamanaji kadhaa katika mji wa kaskazini wa Garoua, ngome ya mpinzani Issa Tchiroma Bakary huku kukiwa na hofu kuhusu uwezekano wa ghasia nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 22, 2025, Waziri wa Mambo ya Ndani Paul Atanga Nji alisema “wasumbufu” waliokamatwa walitumwa na wachochezi kutoka ndani na nje ya nchi.
“Kati ya watu waliokamatwa, 20 watapelekwa katika mahakama za kijeshi kujibu mashataka ya uasi na uchochezi,” Nji alifichua, akiongeza kuwa wengine walipelekwa katika mji mkuu wa Yaoundé kwa uchunguzi zaidi.
Hatua hiyo inafuatia maandamano huko Garoua na Yaoundé ambapo washiriki walishutumu hitilafu za uchaguzi na kueleza kumuunga mkono Tchiroma ambaye alidai ushindi katika uchaguzi wa rais.