Historia mgonjwa wa pili wa Ukimwi akitibiwa na kupona
Na MASHIRIKA
KWA mara ya pili katika historia, madaktari wamefanikiwa kutibu mtu aliyekuwa akiugua ugonjwa wa Ukimwi, baada ya virusi vya HIV ambavyo husababisha maradhi hayo kutokomezwa mwilini mwake.
Habari hizo zimetokea miaka 12 baada ya zingine kama hizo, ambapo mgonjwa mwingine aliripotiwa kutibiwa Ukimwi, japo wanasayansi wamekuwa wakijaribu kutafuta tiba ya maradhi hayo bila mafanikio.
Katika visa vyote viwili, waathirika wa ugonjwa huo wamefanyiwa upasuaji na kubadilishwa uboho wa mwili ili kupona, japo matibabu hayo yalikuwa ya kutibu ugonjwa wa saratani, lakini yakaishia kuponya Ukimwi bila kukusudiwa.
Japo dawa za kudhibiti ugonjwa huo zimekuwepo kwa muda, matibabu ya kubadili viungo vya mwili kama uboho yamekuwa yakihofiwa kuwa hatari kwa afya na kwamba, yanaweza kuwa na athari mbaya kwa mhusika baadaye.
Wataalam, hata hivyo walisema kupanga mwili upya kwa kuweka seli zenye uwezo wa kujikinga kutokana na virusi vya HIV kunaweza kufanikiwa kama matibabu halisi.