Hofu sanamu ya Yesu kutiririkwa na machozi ya damu
BENSON MATHEKA na MASHIRIKA
Acapulco, Mexico
HOFU imezuka nchini Mexico baada ya sanamu moja ya mtoto Yesu kaunza kulia machozi ya damu huku wakazi wakisema ni ishara kutoka kwa Mungu wakomeshe uhalifu na umwagikaji wa damu.
Wakazi wa kijiji cha mashambani cha Kilometro 42 eneo la Acapulco, wanasema kisa hicho kinatokana na ongezeko la ukosefu wa usalama eneo hilo.
Hii ni mara ya nne kwa sanamu hiyo kutokwa na machozi ya damu mwaka huu.
Likinukuu vyombo vya habari vya eneo hilo, gazeti la Mirror lilisema sanamu hiyo ambayo iko katika jengo la kibinafsi ililia machozi ya damu mkesha wa Mwaka Mpya.
Wakazi wanaamini kwamba sanamu hiyo inaonyesha huzuni kutokana na ongezeko la utovu wa usalama.
Visa 111 vya mauaji huripotiwa kwa kila wakazi 100,000 kulingana na shirika la Citizens’ Council for Public Security and Criminal Justice.
Mkazi wa eneo hilo Soledad Natividad Flores aliambia wanahabari kwamba watu wengi wamedai hiki ni kitendo cha shetani japo wengi wanasema ni ujumbe kutoka kwa Mungu.
“Ukweli ni kwamba tumethibitisha inalia hata wakati watu wameishika,” alisema.
Kasisi mmoja alisema wawakilishi wa kanisa Katoliki wanachunguza madai hayo kuhakikisha hakuna mtu atapotosha waumini.