Kimataifa

Hofu ya mapinduzi baada ya wanajeshi kuzua ghasia Mali

August 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

BAMAKO, Mali

WANAJESHI wa Mali Jumanne walizua ghasia katika kambi moja mjini Kati na kuzua hofu ya mapinduzi katika nchi hiyo inayokumbwa na ghasia na kugeuka himaya ya makundi ya kigaidi.

Duru zilisema kwamba wanajeshi walioasi waliwakamata maafisa wakuu wa kijeshi na wa serikali, miezi miwili baada ya nchi hiyo kukumbwa na maandamano raia wakimtaka Rais Ibrahim Boubacar Keita kujiuzulu.

Haikujulikana Rais huyo alikuwa wapi wakati ghasia ziliripotiwa katika kambi hiyo iliyo kilomita 15 kutoka jiji kuu Bamako.

Pia haikujulikana aliyeongoza ghasia hizo lakini kulikuwa na ripoti kwamba maafisa wa serikali walikuwa wamekamatwa.

Wafanyakazi katika ofisi za serikali katika jiji kuu la Bamako pia walihepa baada ya wanajeshi kuanza kuwakamata maafisa wakuu.

“Maafisa wa serikali wanakamatwa. Kuna taharuki kila mahali,” afisa mmoja wa Wizara ya Usalama aliambia wanahabari na kuomba jina lake lisitajwe kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya serikali.

Walioshuhudia walisema vifaru vya wanajeshi na magari yao yalionekana katika barabara za mji wa Kati.

Ubalozi wa Ufaransa ulionya raia wa nchi hiyo katika mji huo na Bamako kutotoka nje.

Matukio ya Jumatatu yalizua hofu ya yaliyotokea kabla ya mapinduzi ya kijeshi ya 2012 ambayo yalitumbukiza Mali katika ghasia.

Mnamo Machi 21, 2012, ghasia zilizuka katika kambi ya kijeshi mjini Kati kabla ya wanajeshi kuvunja hifadhi ya silaha na kuelekea ikulu wakiongozwa na Kapteni Amadou Haya Sanogo.

Baada ya kupindua serikali, Sanongo alilazimishwa na jamii ya kimataifa kukabidhi mamlaka serikali ya mpito ambayo iliandaa uchaguzi mwaka wa 2013 ambao Rais wa sasa Keita alishinda.

Keita anashinikizwa kujiuzulu serikali yake ikilaumiwa kwa kushindwa kuzima makundi ya kigaidi katika nchi hiyo.

Viongozi wa upinzani walikataa wito wa wapatanishi wagawane mamlaka na serikali ya Keita wakisema wanachotaka ni aondoke uongozini.