Kimataifa

Ivory Coast yatisha kuongeza bei ya Cocoa kwa Amerika

Na REUTERS April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

YAMOUSSOUKRO, IVORY COAST

IVORY Coast imeonya kuwa itaongeza bei ya kokwa za kakao – cocoa kwa Kimombo – kwa Amerika iwapo Rais Donald Trump ataendelea na mpango wake wa kuzidisha ushuru kwa bidhaa ambazo taifa lake linaagiza kutoka nje.

Ivory Coast ndiyo huzalisha kakao kwa wingi zaidi duniani; kokwa hizo zikitumika kutayarisha bidhaa mbalimbali za chakula, maarufu zaidi zikiwa ni chokoleti na kiungo cha chai.
Trump aliwekea taifa hilo la Afrika magharibi ushuru wa asilimia 21, kiwango ambacho ni juu zaidi ikilinganishwa na ushuru ambao rais huyo aliwekea nchi zingine jirani za kanda hiyo.
Ingawa hivyo, Trump alitangaza kuwa utekelezaji wa ushuru huo umesitishwa kwa siku 90 kupisha mashauriano zaidi.
Lakini Waziri wa Kilimo wa Ivory Coast, Kobenan Kouassi Adjoumani, Ijumaa alisema hawatacheka na Amerika na ushuru huo lazima usitishwe kabisa.
“Ukitoza ushuru wa juu kwa bidhaa tunayouzia nchi yako, nasi tutaongeza bei ya kakao na mtainunua kwa bei ghali,” akaeleza Kouassi.
Aliongeza kuwa Ivory Coast sasa inalenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Muungano wa Bara Ulaya (EU) ili kuhakikisha inapata soko mbadala.
Hata hivyo, kauli ya waziri huyo inashangaza kwani Ivory Coast haidhibiti bei ya kakao wala haina uwezo kwa sababu bei hutegemea soko la ulimwengu.
Kile Ivory Coast inaweza kufanya ni kuongeza ushuru kwa mataifa yanayonunua kakao zake ili kujizolea mapato zaidi.
Hatua hiyo, hata hivyo, itasababisha bei kuwa juu mno kwa watumiaji bidhaa hiyo nyumbani.
Ivory Coast huuzia Amerika kati ya tani 200,000 – 300,000 za kakao kwa mujibu wa Baraza la Kahawa na Kakao (CCC).