• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:50 AM
Jeshi lazua hofu jijini baada ya Sudan kuondolewa katika AU

Jeshi lazua hofu jijini baada ya Sudan kuondolewa katika AU

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, Sudan

MAAFISA wa usalama waliokuwa na silaha kali waliendelea kuzunguka jiji kuu la Sudan na kufanya wakazi kujifungia ndani ya nyumba saa chache baada ya Muungano wa Afrika kuondoa nchi hiyo kama mshirika wake kufuatia mauaji ya watu 108 yaliyotekelezwa na kikosi maalumu cha wanajeshi.

Wanachama wa kikosi hatari cha Rapid Support Forces, ambacho wanaharakati wanasema kinahusisha wapiganaji wa Janjaweed waliotekeleza mauaji Darfur, walikuwa wakizunguka mjini wakiwa na bunduki za rasharasha kwenye magari, walioshuhudia walisema.

“Tunaishi katika hali ya hofu tele kwa sababu ya milio ya risasi, “ mkazi mmoja wa kusini mwa Khartoum aliambia wanahabari wa AFP.

Alisema hangeruhusu watoto wake kutoka nje kwenda kucheza barabarani. Baraza la kijeshi linalotawala Sudan linaendelea kulaumiwa kwa mauaji hayo huku wizara ya afya ikisema idadi ya waliokufa nchini humo ni 61 wakiwemo watu 52 iliyodai waliuawa kwa kupigwa risasi jijini Khartoum.

Hata hivyo, madaktari wanandai kuwa watu zaidi ya 100 waliuawa wanajeshi walipotawanya waandamanaji waliokuwa wamepiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mnamo Jumatatu.

Chama cha Madaktari nchini Sudan Jumatano kilisema mili 40 ilitolewa mto Nile na kuongeza idadi ya waliouawa kuwa 108.

Chama hicho ambacho ni sehemu ya waandalizi wa maandamano na hutegemea habari kutoka kwa madaktari wanaohudumia watu ilionya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka.

Jeshi lilimpindua rais aliyetawala kwa miaka mingi

Omar al-Bashir mnamo Aprili baada ya maandamano dhidi ya utawala wake kuchacha kwa miezi kadhaa lakini waandamanaji waliendelea kupiga kambi nje ya makao ya jeshi wakitaka utawala wa kiraia.

Mazungumzo kati ya waandalizi wa waandamanaji na baraza la kijeshi yalisabaratika huku waandamanaji wakikataa kutawanyika hadi walipovamiwa na wanajeshi Jumatatu tukio lililolaaniwa kote ulimwenguni.

Hali ya kawaida yaanza kurejea

Hali ya kawaida ilianza kurejea Khartoum Alhamisi kukiwa na maduka machache yaliyofunguliwa na magari machache barabarani.

Lakini katika jiji la Omdurman, wakazi walisema kulikuwa na hofu kubwa kwa sababu ya magari mengi ya wanajeshi waliokuwa na silaha barabarani.

“Ni matumaini yetu kwamba hali hii itaisha haraka ili hali ya kawaida irejee,”mkazi mmoja aliambia wanahabari wa AFP.

Katika uwanja wa ndege wa Khartoum jamaa za wasafiri walikesha wakisubiri ndege zao kuwasili baada ya safari mashirika kadhaa kufutilia mbali safari za ndege zao katika uwanja huo. Hakukuwa na intaneti katika jiji hilo.

Muungano wa Afrika ulitimua Sudan hadi kubuniwe baraza la mpito la kiraia. Muungano huo ulihimiza maafisa wakuu wa jeshi wanaotawala kukabidhi mamlaka baraza la kiraia.

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Sanaa i mishipani na azidi kuipa uhai

Sasa serikali yamtetea Passaris

adminleo