Kutumia simu ukila kutakunenepesha – Utafiti
MASHIRIKA Na PETER MBURU
BRAZIL Na NETHERLANDS
WANASAYANSI sasa wanasema kuwa kutumia simu wakati wa kula kunaweza kumfanya mtu kunenepa sehjemu ya kiuno.
Watafiti wamebaini kuwa watu hula asilimia 15 zaidi ya mafuta wakati wanapoangalia simu wakati wa kula, mbali na kuwa wanaishia kula chakula chenye mafuta zaidi.
Watafiti hao aidha walibaini kuwa kutumia simu wakati wa kula humfanya mtu kutojua kiwango cha chakula ambacho anakula, na hivyo kumfanya kula sana.
“Inaweza kuzuia akili kujua kiwango hasa cha chakula ambacho mtu amekula,” wanasayansi hao, ambao waliwarekodi watu 62 wakila peke yao wakasema.
Watu hao wa kati ya miaka 18 na 28 walihitajika kula chakula walichotaka, vikihusisha vinywaji na chokoleti hadi waridhike.
Katika majaribio matatu, wahusika walihitajika kula bila kusumbuliwa na kitu, wakitumia simu ama kusoma gazeti.
Kwa wastani, walikula kiwango cha mafuta (calories) cha 535 bila kutumia simu, lakini walipokuwa wakitumia simu wakala kiwango cha 591 cha calories.
Watu waliokuwa wanene katika kikundi hicho walikula kiwango cha 616 cha Calories walipokuwa wakitumia simu. Wakitumia simu, wahusika aidha walitumia asilimia 10 zaidi ya vyakula vyenye mafuta, na kula zaidi walipokuwa wakisoma magazeti.
“Matumizi ya simu ‘Smartphone’ wakati wa kula yaliongeza kiwango cha Calories na ulaji wa vyakula vya mafuta,” akasema Marcio Gilberto Zangeronimoa ambaye alikuwa mkuu wa utafiti huo, uliofanywa katika vyuo kikuu vya Lavras, Brazil na cha kimatibabu cha Utrecht, nchini Netherlands.
Watafiti walisema kuwa simu za smartphone zimekuwa kitu kinachoathiri watu wakati wanapokula, hivyo wakitaka watu kuwa makini wanapochagua chakula wakati wanatumia simu.
“Zinazuia akili kuelewa vyema kiwango cha chakula ambacho mtu ametumia,” wakasema.
Utafiti huo umechapishwa katika jarida la Physiology And Behavior.