Machar kutia saini mkataba wa amani na Salva Kiir
MASHIRIKA Na PETER MBURU
HATIMAYE kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar alikubali kutia saini mkataba wa maelewano ya amani na Rais Salva Kiir, baada ya kudinda mbeleni, ripoti kutoka taifa hilo zilisema.
Ripoti zilisema Bw Machar aliahidi kufanya hivyo Alhamisi, Agosti 30 baada ya matakwa waliyolalamika kuhusu kurekebishwa kwenye mkataba wa maelewano.
Hii ni baada ya wiki kadha za mazungumzo kati ya Rais Kiir na Bw Machar Jijini Khartoum, Sudan ya juu, wakitafuta muafaka ili kumaliza vita, ambavyo vimeua maelfu ya wananchi na mamilioni kuhama makwao tangu 2013.
Pande zote mbili zimekuwa zikishiriki mazungumzo ya aina hiyo, yakihusisha kumaliza vita na kugawana mamlaka ambapo Bw Machar amekuwa akiishia kuwa makamu wa rais.
Lakini Jumanne asubuhi, mazungumzo hayo yalionekana kupata pigo wakati Bw Machar alidinda kutia saini maelewano, licha ya Juba kukubaliana nayo.
“Pande kuu za upinzani wa Sudan Kusini, zikiwemo SPLM-IO (kikosi cha Machar) zilikataa kutia saini makubaliano ya mwisho, zikitaka matakwa yao kuwekwa,” akasema waziri wa maswala ya nje Sudan Al-Dierdiry Ahmed awali Jumanne.
Lakini baadaye, wapatanishi walitangaza kuwa Bw Machar alikubali kutia saini.
“Baada ya mazungumzo ya kina na wapatanishi wa Sudan Kusini, Riek Machar alikubali kutia saini karatasi hiyo Alhamisi Agosti 30,” akasema waziri Ahmed.
Ilisemekana Machar na wenzake walikuwa wakikataa kutia saini kwa kuwa matakwa yao hayakujumuishwa katika mkataba huo wa maelewano.
Baadhi ya mambo wanayozozania ni kuhusu namna serikali inayopendekezwa itafanya kazi, majimbo ambayo taifa hilo litakuwa nayo na kuhusu kutengenezwa kwa katiba mpya.