Madai Michael Jackson aliwadhulumu watoto kingono yazua ghadhabu
MASHIRIKA Na PETER MBURU
MASHABIKI wa aliyekuwa msanii tajika kutoka Marekani, marehemu Michael Jackson wameghadhabishwa na habari ya upekuzi inayodai kuwa msanii huyo alikuwa na tabia ya kuwadhulumu kingono wavulana wachanga.
Makala hayo, Leaving Neverland, ambayo yalichezwa Ijumaa katika ukumbi wa filamu wa Park City, Utah yanawahusisha wanaume wawili wanaodai kuwa walidhulumiwa na msanii Jackson, Bw Wade Robson na James Safechuck. Walisema kuwa uhusiano wao kingono na Jackson ulikuwepo walipokuwa wavulana wachanga.
Baada ya ‘ufichuzi’ huo mashabiki wa Michael Jackson wamekashifu Robson na James, na kuyapa Makala yenyewe jina ‘Liar’ (muongo), mwanaume asiyeweza kusema ukweli.
Mashabiki hao wanadaiwa kupenyeza katika akaunti ya mtandao wa filamu wa IMDb Ijumaa na kubadili jina la Makala kuwa ‘Liar, Liar 2: The Wade Robson and Jimmy Safechuck story.’
Baadhi ya watu walidai kuwa wawili hao ambao kwenye Makala wanadai Jackson aliwadhulumu kingono mbeleni waliwahi kupinga madai hayo.
Baada ya saa chache za mkanganyiko, ukurasa wa IMDb ulibadilishwa na kusoma jina la filamu ‘Leaving Neverland.’
Familia ya Jackson ilipuuzilia mbali filamu hiyo na kuitaja kuwa vita vya kumchafua shujaa huyo wa muziki, wakisema alihangaishwa akiwa hai na hadi sasa akiwa maiti.
Robson na Safechuck kwa muda mrefu wamekuwa wakidai kuwa walidhulumiwa na mwanamuziki huyo katika boma lake la Neverland ranch.
Wasimaizi wa biashara za Michael Jackson Ijumaa usiku walikosoa filamu hiyo kwa “kuchapisha madai yasiyokuwa na ushahidi na yanayoaminika kutendeka miaka 20 iliyopita, kisha kuyafanya kuwa kama ya kweli.”
Waliwataja Robson na Safechuck kama waongo pia, wakisema kuwa Michale Jackson alipokuwa hai, walitoa habari kuwa hakuwadhulumu.
“Filamu hiyo inachukua madai ya uongo yanayoaminika kutendeka miaka 20 iliyopita na kuyafanya kama ya kweli,” ujumbe wa wasimamizi wa mali ya Jackson ukasema.
“Madai haya ndiyo yalikuwa msingi wa kesi zilizofikishwa kortini na waongo hawa wawili na zikatupwa na jaji,” ujumbe huo ukasema.
“Wawili hao walitoa ushahidi wa kiapo kuwa matukio hayo hayakuwahi kufanyika. Hawajatoa ushahidi wowote kuhusu madai yao.”
Filamu hiyo ya saa nne inamkosoa msanii huyo aliyesifika, kwa kutumia harusi baina yake na mvulana mchanga.
“Kati ya ufichuzi mwingi uliowahi kutolewa wa kutisha kuhusu #LeavingNeverland: MJ alimpa mmoja wa wavulana wadhulumiwa kifaa cha pambo ili wafanye ngono n ahata kuandaa harusi ya kejeli, ikiwa na viapo na pete,” akasema Patrick Ryan wa USA Today.
Filamu hiyo inatarajiwa kucheza katika shoo za Grammy na vituo vya HBO na Channel 4 UK.
Kabla ya kifo chake, Jackson alipinga madai yote kuwa aliwadhulumu kingono wavulana wadogo, na familia yake imekuwa ikishikilia kauli hiyo hata baada yake kufa.