Magufuli akosa mkutano wa njia ya video wa EAC kujadili Covid-19
Na CHARLES WASONGA
KWA mara nyingine Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amekosa kuhudhuria mkutano wa marais wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) kwa njia ya video wa kujadili janga la Covid-19.
Katika mkutano wa Jumanne uliofanyika kwa njia ya mtandao, waliohudhuria ni marais Uhuru Kenyatta (Kenya), Paul Kagame (Rwanda), Salva Kiir (Sudan Kusini) na Yoweri Museveni wa Uganda.
Mwenendo wa Rais Magufuli wa kukosa mikutano ya EAC ya kujadili janga hili umeibua hisia kali wakati huu ambapo serikali yake imekataa kuweka masharti kama ya nchi wanachama ya kuzima kusambaa kwa virusi vya corona.
Hali hii, baadhi ya wataalamu wamesema, imesababisha ongezeko la visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini humo.
Kufikia Jumatatu, Tanzania ilikuwa imethibitisha visa 509 vya maambukizi na vifo 21 kutokana na ugonjwa huo.
Miongoni mwa waliofariki kutokana na ugonjwa huo hatari ni wabunge wawili wanaohudumu sasa na wawili wa zamani.
Mkutano wa marais wa mataifa wanachama wa EAC unajiri wakati ambapo kumeibuka hofu kuhusu ongezeko la visa vya maambuzi karibu na maeneo ya mipaka ya mataifa hayo.
Kwa mfano, mnamo Jumatatu, Kenya iligundua visa tisa miongoni mwa madereva wa matrela katika mji wa Namanga ulioko katika mpaka wake na Tanzania.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi pia hakushiriki katika mkutano wa Jumanne.
Taifa hilo linajiandaa kwa uchaguzi wa urais juma lijalo.
Katika mkutano wa Jumanne, Rais Kenyatta amehimiza ushirikiano baina ya mataifa yao waweze kushinda vita dhidi ya kusambaa kwa virusi vya corona.
“Tunapasa kuungana pamoja kushinda changamoto hii kwa sababu mipaka yetu ni penyevu,” akasema.
Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga, katika mahojiano yake ya shirika la habari la Uingereza (BBC) majuzi, alisema kuwa Rais Magufuli hajakuwa akizungumza na viongozi wa ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Bw Odinga na Magufuli ni marafiki wa karibu ambao wamekuwa wakishirikiana katika masuala ya kisiasa na kibinafsi kwa muda mrefu.
“La, sijakuwa nikizungumza na rafiki yangu. Nilijaribu kumfikia kwa kumpigia simu, lakini sikufaulu,” akasema.
“Kwa hivyo, nimemtumia ujumbe mfupi,” Bw Odinga akaongeza.
Mkutano huo wa marais wa EAC pia ulijadili suala la kuwezesha usafirishaji wa bidhaa na mikakati ya kudhibiti homa ya corona.
Mkutano huo uliitishwa na kuongozwa na Rais Kagame ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya EAC.
Marais hao walishukuru washirika wa maendeleo wakiwemo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Taasisi ya Afrika Kuhusu Udhibiti wa Magonjwa (Africa CDC) kwa kuendelea kuyasaidia mataifa ya Afrika Mashariki kupambana na virusi vya corona.