Maiti za waliokufa Tanzania kufanyiwa uchunguzi wa DNA
NA AFP
SERIKALI ya Tanzania Jumatatu ilitangaza kuanzishwa kwa uchunguzi wa DNA kwenye miili iliyoteketea hadi kiwango cha kutotambulika, katika ajali ya lori la mafuta iliyowaangamiza watu 71 mjini Morogoro wikendi.
Waziri wa Masuala ya Bunge, Jenista Mhagama alisema familia ambazo miili ya wapendwa wao itakuwa imetambuliwa zitakuwa huru kuichukua na kuizika wakati wowote.
“Baadhi ya walioaga dunia na manusura tayari wametambuliwa. Tunataka kuhakikisha kwamba yeyote aliyehusika kwenye janga hili anatambuliwa,” akasema Bi Mhagama.
Waziri huyo pia alisema kitengo spesheli cha kutoa ushauri nasaha kwa walioathirika kisaikolojia na janga hili kimeundwa na kinaendelea kutekeleza jukumu lake.
Huku hayo yakiendelea, serikali pia ilitangaza kuundwa kwa tume ya uchunguzi kuangazia namna asasi za serikali zilivyojitokeza na kukabiliana na janga hilo kwa lengo la kuwaokoa waliokuwa wakiungua.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa tangazo hilo mjini Morogoro mnamo Jumapili alipoongoza ibada ya mazishi ya baadhi ya walioangamia.
Bw Majaliwa aliwaambia waombolezaji kwamba tume hiyo, ambayo wanachama wake watatajwa baadaye, itahitajika kuwasilisha mapendekezo yake kufikia Ijumaa wiki hii.
“Tunatarajia kupata ripoti yenye maelezo ya kina ambayo itatoa mwanga kuhusu hatua itakayochukuliwa na serikali baadaye,” akasema Bw Majaliwa.
Waziri huyo mkuu aliongeza kwamba lengo kuu la uchunguzi huo ni kufahamu jinsi ambavyo asasi husika zilivyojitokeza huku maswali mengi yakizidi kuzuka kuhusu jinsi janga hilio baya zaidi kuwahi kushuhudiwa Tanzania lilivyotokea na kusababisha vifo.
“Ajali hiyo ilitokea saa mbili asubuhi katikati mwa manispaa. Ilifanyika wakati watumishi wa umma walikuwa kazini. Tunataka kujua iwapo walikuwa kazini kwa ukweli na nani anafaa kulaumiwa,” akaongeza Bw Majaliwa.
Alisema serikali na umma ingependa kujua polisi na magari ya wazimamoto yalichukua muda gani kuwasili katika eneo la ajali.
Pia alishangaa kwa nini watu waliobeba mitungi na ndoo waliruhusiwa kung’ang’ana kuchota mafuta kwenye lori hilo, ilhali ilikuwa wazi walikuwa wakihatarisha maisha yao.
“Tunataka kujua iwapo kulikuwa na afisa wa usalama ambaye alipaswa kuwazuia watu kuteka mafuta kwenye lori hilo lakini hakuwajibika,” akasema Bw Majaliwa.
Kufikia jana, idadi ya vifo ilikuwa imefika 71 huku majeruhi 59 nao wakiendelea kutibiwa katika hospitali ya Kitaifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam pamoja na nyingine katika miji ya Morogoro na Dodoma.