Makamu rais Machar anayezuiliwa kuchunguzwa na kuchochea uasi Sudan Kusini
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, ambaye amekamatwa, anachunguzwa kwa tuhuma za kuchochea uasi, serikali ya nchi hiyo ilitangaza Ijumaa, ikithibitisha kwa mara ya kwanza kukamatwa kwake ambako kumeibua hofu ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ripoti kwamba Machar – ambaye ni mpinzani wa muda mrefu wa Rais Salva Kiir – alikamatwa Jumatano zilisababisha miito kutoka jamii ya kimataifa ya utulivu kudumishwa. Kenya, ambayo ni jirani, ilimtuma Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, kujaribu kutuliza hali.
Chama cha Machar kilisema wiki hii kwamba kukamatwa kwake kulifuta makubaliano ya amani ya 2018. Makubaliano hayo yalimaliza vita vya miaka mitano kati ya vikosi vya Dinka vinavyomuunga mkono Kiir na wapiganaji wa Nuer waliokuwa waaminifu kwa Machar.
Msemaji wa serikali na Waziri wa Habari, Michael Makuei, alisema katika taarifa yake kwamba “Machar na wenzake wa SPLM/A-IO, ambao wanapinga amani na wako kizuizini, watachunguzwa na kufikishwa mbele ya sheria ipasavyo.”
Alishutumu Machar kwa kuwasiliana na wafuasi wake na “kuwachochea waasi dhidi ya serikali kwa lengo la kuvuruga amani ili uchaguzi usifanyike na Sudan Kusini irudi vitani.”
“Makubaliano ya amani hayajaporomoka na hayataporomoka kwa hali yoyote,” Makuei alisema.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa Machar au chama chake kuhusu madai hayo.
Chama cha Machar hapo awali kilikanusha madai ya serikali kwamba kinaunga mkono Jeshi Jeupe, kundi la wanamgambo wa kabila la Nuer, ambalo lilipigana na jeshi katika mji wa kaskazini mashariki wa Nasir mwezi huu, na kusababisha mzozo wa sasa.
Kutokana na mapigano hayo, vikosi vya Kiir vilikamata washirika kadhaa wa Machar, wakiwemo Waziri wa Mafuta na naibu mkuu wa jeshi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema Ijumaa kuwa mchakato wa amani umevurugika na akawataka viongozi wa Sudan Kusini kuweka silaha chini na kuweka maslahi ya wananchi mbele.
“Tusifiche maneno: Tunachokiona kinarejesha kumbukumbu za vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013 na 2016 ambavyo viliua watu 400,000,” Guterres alisema.
Rais wa Kenya, William Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema alizungumza na Kiir kuhusu kukamatwa kwa Machar.
Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, alisema kwenye X kuwa alikutana na Kiir Ijumaa na alitiwa moyo kwamba kuna uwezekano wa mgogoro huo kutatuliwa. Aliongeza kuwa baadaye alisafiri kwenda Uganda kwa mkutano na Rais Yoweri Museveni.
Mataifa ya Magharibi, yakiwemo Amerika, Uingereza na Ujerumani, yamefunga balozi zao au kupunguza shughuli zao Sudan Kusini.
Wachambuzi wa siasa wanasema Kiir amekuwa akijaribu kuimarisha nafasi yake kwa kuwakamata washirika wa karibu wa Machar, kuwaalika wanajeshi wa Uganda na kumteua mshauri wake, Benjamin Bol Mel, kuwa makamu wa pili wa rais.