Kimataifa

Makamu Rais wa Sudan Kusini Machar akamatwa

Na REUTERS,HAPPINESS LOLPISIA March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

AMERIKA mnamo Alhamisi Machi 27 ilitoa wito kwa Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, kumuachilia mpinzani wake, Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, ambaye inasemekana amezuiliwa nyumbani, ikisema  viongozi wa nchi hiyo wanafaa kuonyesha kujitolea kwao kwa amani.

Chama cha Machar cha SPLM-IO kilisema siku ya Jumatano kuwa waziri wa ulinzi na mkuu wa usalama wa taifa “waliingia kwa nguvu” katika makazi ya Machar na kumpa kibali ya kukamatwa kwake.

Machar alishikiliwa nyumbani kwake pamoja na mkewe na walinzi wake wawili, akituhumiwa kuhusika katika mapigano kati ya jeshi na kundi linalofahamika kama Jeshi Jeupe huko Nasir, jimbo la Upper Nile mwezi huu, kulingana na taarifa ya Reath Muoch Tang, afisa mwandamizi wa SPLM-IO, iliyoonwa na Reuters siku ya Alhamisi.

“Tunatiwa wasiwasi na ripoti kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Machar, amewekwa chini ya kifungo cha nyumbani,” Ofisi ya Masuala ya Afrika ya Washington iliandika kwenye X.

“Tunamtaka Rais Kiir abadilishe hatua hii na kuzuia kuzorota zaidi kwa hali hiyo.”

Chini ya makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013-2018 kati ya vikosi vya Machar kwa upande mmoja na vile vya Kiir kwa upande mwingine, Sudan Kusini ina manaibu rais watano. Mpinzani wa muda mrefu wa Kiir na kiongozi wa upinzani, Machar, kwa sasa anahudumu kama makamu wa kwanza wa rais.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mapigano ya hivi punde huko Nasir kati ya jeshi na Jeshi Jeupe, kundi la wanamgambo lenye uhusiano wa kihistoria na Machar, pamoja na kuongezeka kwa hotuba za chuki, yanaweza kuchochea tena vita vya kikabila vilivyomalizika mwaka 2018.

Chama cha Machar cha SPLM-IO kimekana kuwa na uhusiano wowote unaoendelea na Jeshi Jeupe.

“Ni wakati ambao viongozi wa Sudan Kusini wanafaa kuonyesha ukweli wa ahadi zao kwa amani,” Ofisi ya Masuala ya Afrika ya Washington iliandika kwenye X.

Jeshi la Sudan Kusini na wasemaji wa serikali hawakujibu mara moja maombi ya kutoa maoni.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa makubaliano ya amani, ambayo yamewawezesha Kiir na Machar kuhudumu katika serikali ya muungano dhaifu, yako hatarini kuvunjika.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini (UNMISS) kimeitaka serikali kuwa na busara, kikisema kuwa viongozi wa nchi hiyo wako ukingoni  kurejea katika mgogoro.

“Hili halitaathiri tu Sudan Kusini, bali pia litaleta madhara kwa eneo zima,” UNMISS ilisema katika taarifa yake.

Mapema mwezi huu, serikali ya Kiir iliwakamata maafisa kadhaa wa chama cha Machar, wakiwemo waziri wa mafuta na naibu mkuu wa jeshi, kufuatia mapigano na Jeshi Jeupe katika Jimbo la Upper Nile.

Siku ya Jumatano, Umoja wa Mataifa uliripoti mapigano kati ya vikosi vya Kiir na Machar karibu na mji mkuu, Juba.