Kimataifa

Mchina aponea kifo baada ya kujidunga sindano ya juisi kuboresha afya

March 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMKE kutoka China alikuwa karibu kufa, baada ya kujidunga sindano zenye zaidi ya aina 20 za sharubati za matunda kwenye mishipa, ili kuinua afya yake.

Mwanamke huyo kwa jina Zeng, wa miaka 51, anaripotiwa kuwa alidhani kwa kujidunga juisi za matunda mwilini moja kwa moja angejipa afya nzuri lakini muda mfupi tu baada ya kujidunga akaanza kuwashwa na ngozi na kuhisi baridi.

Alikimbizwa katika hospitali ya Chenzhou katika mkoa wa Hunan mnamo Februari 22, kisha akahamishwa katika hospitali zingine mbili, ambapo alilazwa eneo la wagonjwa mahututi.

Daktari aliyemtibu Liu Jianxiu aliambia wanahabari kuwa mwanamke huyo alianza kuathirika moyo, figo na ini.

Alikuwa katika hatari ya kufa baada ya sehemu kadhaa za mwili kushindwa kufanya kazi, akasema daktari huyo.

Madaktari walimpa dawa za kuosha damu na baada ya siku kadhaa za matibabu ya dharura hali yake ikaanza kuboreka.

Maafisa wa hospitali walieleza wanahabari kuwa mwanamke huyo alikuwa amemwita daktari nyumbani kwake kumdungia juisi za matunda hayo mwilini, baada ya kujifanya kuwa mgonjwa. Hata hivyo, daktari alipoondoka, alichanganya dawa aliyoachiwa na juisi ya matunda na kujidunga.

“Nilidhani matunda yana afya nzuri na sikudhani yangenidhuru kwa kujidunga,” akasema Zeng.