Kimataifa

Mhubiri ajitetea kuwataka waumini wamnunulie ndege ya Sh5.4 bilioni

June 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na VALENTINE OBARA 

NEW ORLEANS, AMERIKA

MHUBIRI aliyeambia waumini wake wamnunulie ndege mpya ya kifahari amejitetea na kusema wanaomkosoa hawakumwelewa.

Mhubiri huyo mashuhuri, Jesse Duplantis, alisema uamuzi wake kutaka anunuliwe ndege inayogharimu dola milioni 54 (Sh5.4 bilioni) ulitokana na hitaji la kueneza injili zaidi.

Video iliyosambazwa awali mitandaoni ilimwonyesha akisema: “Kama Yesu Kristo angelikuwa ulimwenguni hii leo, hangekuwa akisafiri kwa punda. Angekuwa anasafiri kwa ndege kote ulimwenguni.”

Matamshi hayo yalikashifiwa na wengi ambao walionelea hizo ni tamaa za kidunia zisizopaswa kuonekana kwa watumishi wa Mungu, hasa ikizingatiwa mhubiri huyo alisemekana tayari anamiliki ndege tatu.

Kwa kujitetea alisema: “Watu hawakunielewa. Nilisema nimewahi kumiliki ndege tatu, sio kwamba nina ndege tatu hivi sasa. Mbili zinatumika katika misheni tofauti na ninamiliki moja pekee kwa sasa.”

Mashirika ya habari yalimnukuu kusema kwamba atapeana ile aliyo kwa sasa ili ikatoe misaada endapo atanunuliwa jipya.

Wahubiri wengine Amerika ambao wamewahi kugonga vichwa vya habari kwa utajiri wao mkubwa ni Joel Osteen na Kenneth Copeland.