Kimataifa

Misri yakana dai la kuiba viungo vya maiti ya mtalii

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Mashirika

SERIKALI ya Misri imekanusha madai kwamba iliiba viungo vya mwili wa mtalii raia wa Uingereza, aliyefariki katika hali ya kutatanisha alipokuwa likizoni.

Maiti ya mtalii huyo ilisafirishwa nchini Uingereza kutoka Misri bila baadhi ya viungo.

David Humphries (pichani), 62, alifariki mnamo Septemba 18 alipokuwa akivinjari katika hoteli ya Hurghada iliyoko katika ufukwe wa Bahari Nyekundu.

Maiti hiyo ilipowasili Uingereza serikali iliifanyia upasuaji na ikabainika mwili huo haukuwa na moyo, maini na figo.

Serikali ya Misri ilipuuzilia mbali ripoti hiyo ya upasuaji huku ikisema kuwa haina mashiko.

Misri ilisema kuwa viungo hivyo viliondolewa wakati wa upasuaji wa kubainisha chanzo cha kifo cha mtalii huyo lakini haikutoa sababu kwa nini havikurudishwa.

Inasadikiwa kuwa huenda mtalii huyo alifariki kutokana na shinikizo la damu.