Kimataifa

Moto waua 25, wakiwemo watalii katika kilabu maarufu

Na BENSON MATHEKA, MASHIRIKA December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MOTO uliotokea katika kilabu maarufu cha usiku katika eneo la pwani la Goa nchini India umeua watu 25, maafisa wa eneo hilo wamesema.

Polisi wanaamini kuwa mtungi wa gesi ulilipuka jikoni katika kilabu cha Birch, kilichoko karibu na ufukwe maarufu. Ukumbi huo ulikuwa umefurika wateja waliokuwa wamefika kumsikiliza DJ wa Bollywood.

Watu wanne wa familia moja kutoka Delhi na wafanyakazi 21 walikuwa miongoni mwa waathiriwa, polisi wa Goa walisema, wakiongeza kuwa wengi walifariki kutokana na kukosa hewa.

Meneja wa kilabu hicho amekamatwa na hati ya kukamatwa kwa mmiliki wake imetolewa.

Goa ni koloni ya zamani ya Ureno pwani ya Bahari ya Arabia. Maisha yake ya usiku, fukwe za mchanga na hoteli huvutia mamilioni ya watalii kila mwaka.

Walioshuhudia waliambia BBC kuhusu hali ya taharuki katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za usiku.

Mmoja alisema alikuwa nje ya klabu hiyo katika usiku wa kawaida wa Jumamosi huku watalii wakijivinjari pale aliposikia mayowe.

“Sikuelewa kilichokuwa kinaendelea mwanzoni,” alisema.

“Baadaye ikawa wazi kuwa moto mkubwa ulikuwa umewaka. Hali ilikuwa ya kutisha sana.”

Ingawa mlango mkuu ni mpana, daraja dogo linalovuka ziwa dogo kuelekea jengo kuu ni jembamba, jambo lililowafanya wazima moto washindwe kufika kwa urahisi eneo la tukio.

Kamanda wa polisi wa eneo hilo, Alok Kumar, alisema moto ulikuwa umeenea zaidi katika eneo la jikoni kwenye ghorofa ya chini.

Waziri mkuu wa Goa, Pramod Sawant, aliwaambia wanahabari kuwa watu watatu walifariki kwa moto kuwachoma, huku wengine wakifariki kutokana na kukosa hewa. Watu wengine sita wako katika hali thabiti hospitalini.

Maafisa walisema wafanyakazi 20 waliokufa walitoka majimbo ya India ya Jharkhand, Uttarakhand, Maharashtra, Assam, Uttar Pradesh, West Bengal na Karnataka. Mfanyakazi mmoja alitoka Nepal.

Walisema kuwa waathiriwa wengine wanne walikuwa watalii kutoka Delhi.

Mpishi anayefanya kazi katika ukumbi jirani aliambia BBC kuwa aliwafahamu baadhi ya wafanyakazi wa klabu ya Birch.

“Watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na pia kutoka Nepal hufanya kazi katika kumbi tofauti za starehe huko Goa,” alisema.

“Nina wasiwasi sana kuhusu baadhi ya watu niliowafahamu kwenye klabu hiyo. Simu zao hazipatikani.”

Jumapili, vikosi vya uokoaji vilikuwa vikichunguza mabaki yaliyoteketea.

Uchunguzi kuhusu chanzo cha moto umezinduliwa, waziri mkuu alisema.

“Wale watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua kali zaidi kisheria – uzembe wowote utashughulikiwa vikali,” Dkt Sawant aliongeza.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alitaja moto wa Goa “wa kuhuzunisha sana” katika ujumbe alioweka kwenye mitandao ya kijamii.