Kimataifa

Mtambue rais wa kwanza mwanamke Ethiopia

October 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

BBC na PETER MBURU

ETHIOPIA kwa mara ya kwanza imepata Rais mwanamke, baada ya wabunge wa nchi hiyo kumchagua Bi Sahle-Work Zewde, kufuatia hatua ya aliyekuwa Rais Mulatu Teshome kujiuzulu.

Bi Sahle-Work, ambaye ni mwanadiplomasia wa miaka mingi na aliyehudumu katika Umoja wa Mataifa (UN) alichaguliwa Alhamisi.

Kuchaguliwa kwake kumekuja wiki moja tu baada ya Waziri Mkuu wan chi hiyo Abiy Ahmed kuteua baraza la mawaziri lenye nusu ya wanawake.

Hata hivyo, kiti chake hicho hakina nguvu za kikweli kwani ni Waziri Mkuu aliye na mamlaka ya Kirais ikilinganishwa na mataifa mengine.

Katika hotuba yake baada ya kuchaguliwa, Bi Sahle-Work alizungumza kuhusu umuhimu wa kudumisha amani.

Rais huyo mpya mbeleni amehudumu kama balozi wa Ethiopia Senegal na Djibouti, mbali na kuhudumu katika nafasi kadha katika UN, ikiwemo mkuu wa kukuza amani taifa la Congo ya Kati (CAR).

Lakini hadi kuchaguliwa kwake, Bi Sahle-Work alikuwa mwakilishi wa UN katika Umoja wa Afrika (AU).

Kulingana na katiba ya Ethiopia, kiti cha Urais huwa hakina nguvu kama cha Waziri Mkuu ambaye ndiye mwenye mamlaka.