• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Mugabe aendelea kutibiwa nchini Singapore

Mugabe aendelea kutibiwa nchini Singapore

Na AFP na MARY WANGARI

ALIYEKUWA Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, 95, bado anaendelea kutibiwa katika hospitali moja nchini Singapore ambapo amekuwa akipokea huduma za afya kwa muda wa miezi minne sasa.

Mugabe amekuwa akipokea huduma za matibabu kuhusiana na ugonjwa ambao haujafichuliwa na alikuwa akipata nafuu kutokana na matibabu kwa mujibu wa mrithi wake, Rais Emmerson Mnangagwa, kupitia taarifa mnamo Jumatatu.

“Rais Robert Mugabe angali katika hospitali mojawapo Singapore ambapo anapokea huduma za kimatibabu. Kinyume na hapo zamani ambapo angehitaji karibu mwezi mmoja tu kwa shughuli hii, madaktari wake safari hii waliagiza atazamwe kwa makini kwa muda mrefu zaidi kuanzia Aprili 2019 alipoondoka kufanyia ukaguzi wake wa kimatibabu hivi majuzi,” alisema Mnangagwa.

Mnangagwa aliyetangaza mnamo Novemba 2018 kwamba Mugabe hakuwa akiweza kutembea kwa sababu ya afya yake kuzorota na kukonga kiumri, alisema alikuwa ametuma timu akiwemo Katibu Mkuu wa Baraza Bw Misheck Sibanda nchini Singapore wiki iliyopita ili kumjulia hali kiongozi huyo wa zamani.

“Nina furaha kuu kulifahamisha taifa kwamba aliyekuwa rais anaendelea kupiga hatua imara katika kupata nafuu hatimaye na kwamba hali yake ni thabiti kwa umri wake,” alisema.

Kundi lililomtembelea Mugabe liliripoti kwamba alikuwa “akipata nafuu vyema kutokana na matibabu” na kwamba “kwa sababu ya jinsi alivyokuwa akiendelea vyema (mwenzetu) Mugabe huenda akaachiliwa hivi karibuni.”

Serikali ilipotangaza mnamo Aprili kwamba alikuwa amesafiri Singapore kupokea matibabu, ilisema kuwa alitarajiwa kurejea katikati mwa Mei.

Huduma za afya ya umma nchini Zimbabwe zimesambaratika na wale wanaojimudu kifedha hutafuta matibabu Afrika Kusini au kwingineko ughaibuni.

Wakati wa hatamu yake uongozini, Mugabe alipokea karibu huduma zake zote za afya nchini Singapore.

Mnangagwa alichukua usukani mnamo Novemba 2017 akiungwa mkono na jeshi na kukatiza utawala wa Mugabe uliodumu miaka 37. Kisha alichaguliwa katika uchaguzi uliopingwa mnamo Julai 2018.

Ameahidi kufufua uchumi wa Zimbabwe uliosambaratika kwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka mataifa ya kigeni unaohitajika mno, lakini miezi michache tu baada ya kuchaguliwa kwake, zimwi la masaibu ya kiuchumi limerejea kuhangaisha taifa hilo ikiwemo uhaba wa mikate, mafuta na umeme kukatwa kwa hadi muda wa saa 18.

You can share this post!

KILIMO: Ukuzaji wa vitunguu saumu

Nitatetea kiti changu 2022 – Gavana Mumbi Kamotho

adminleo