Mwanamke aliyepelekwa mochari akiwa hai afariki hospitalini
MASHIRIKA Na PETER MBURU
POLISI nchini Urusi wanachunguza kisa ambapo mwanamke wa miaka 62 alifikishwa mochari akiwa hai, baada ya kudaiwa kufa, lakini mfanyakazi wa mochari akabaini kuwa alikuwa hai.
Inadaiwa kuwa mwanamke huyo kutoka eneo la Amur, Russia alikuwa akisherehekea pamoja na watu wa familia yake, wakati waliugua na kuonekana kama aliyekufa.
Watu waliwaita polisi, ambao pia nao ‘walidhibitisha’ kuwa ni kweli hakuwa hai, ripoti zikasema.
Lakini alipofikishwa katika chumba cha kuhifadhi maiti, mfanyakazi aliyekuwa akimhudumia alibaini kuwa alikuwa uhai, kwani alianza kusonga songa alipodungwa kifaa cha kumbainisha mguuni.
Mfanyakazi huyo aliita ambulensi mara moja na madaktari wakatumia dakika 40 kujaribu kumwamsha, japo hakuamka.
Kulingana na daktari mkuu wa hospitali ya Belogorsk Mikhail Danilov, mwanamke huyo alikuwa ameadhirika na baridi kali.
Alipofikishwa hospitalini, alilazwa eneo la wagonjwa mahututi, lakini kwa bahati mbaya akafa siku iyo hiyo, kutokana na ugonjwa wa ‘Hypothermia’, wizara ya afya ikasema.
Lakini madaktari walisema kuwa endapo angepelekwa hospitalini na kupokea matibabu ya haraka badala ya kupelekwa mochari, huenda angepona.
Kutokana na hayo, polisi wameanzisha uchunguzi dhidi ya kisa hicho.
Afisa wa afya alisema kuwa afisa wa polisi aliyedai mwanamke huyo ameaga dunia alikiuka kanuni kwani angeitisha msaada wa ambulensi ili madaktari wakamkague.
“Alidhibitisha kifo kivyake, akaita watu wa mochari na kutuma mwili mochari bila nakala za kudhibitisha,” akasema afisa huyo.