Kimataifa

Mwanamke aliyezaliwa bila uke aomba msaada kupata watoto

February 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMKE kutoka Canada ambaye alizaliwa bila sehemu nyeti na utumbo wa mtoto anajikaza kuchangisha zaidi ya Sh9 milioni, ili aweze kutibiwa jinsi ataanzisha familia pamoja na mumewe.

Sarah Giesbrecht wa miaka 21 kutoka Simcoe, Ontario aligundua kuwa alikuwa na tatizo la kiafya wakati alifikisha miaka 16, bila kupata hedhi, japo madaktari walipuuza kuwa hakikuwa kitu kikubwa.

Lakini baada ya miaka miwili mingine kupita katika hali hiyo, alianza kwenda kwa madaktari mara kwa mara kupimwa, ndipo akapatikana na ugonjwa wa Mayer-Rokitansky-Küster-Hauser syndrome (MRKH).

Aliambiwa na madaktari kuwa hawezi kuzaa kutokana na hali hiyo, na akaanza kuwaza sana.

Kutokana na hayo, mwanmke huyo ameanza kuchangisha pesa ili kugharamia matibabu ya hali hiyo ya utasa, ili aweze kutumia mbinu ya IVF kupata mtoto.

“Nilipoenda kwa daktari mara ya kwanza nilipokuwa na miaka 16, daktari alinifanya kuhisi kama hakikuwa kitu kikubwa, kuwa kulikuwa na muda wa kutosha kurekebisha hali,” akasema Sarah.

“Baada ya kupimwa miaka miwili baadaye, niliambiwa kuwa sina utumbo wa kubeba mtoto,” akasema. “Nilianza kufikiria kuwa sitawahi kuwa mama na sitawahi kupata watoto, nililia sana.”

Alisema kuwa wakati huo alikuwa na mpenzi na pamoja walitaka kuwa na watoto, jambo ambalo lilikwazwa mara moja.

“Kupata watoto lilikuwa lengo langu kuu na hivyo kuanza kuambiwa mambo ya kupinga hivyo ilikuwa vigumu kwangu kuelewa.”

Baada ya kuwaza kwa pamoja na mpenzi wake, waliamua badala ya kumchukua mtoto asiye wao wakamlea watumie mbinu ya kisayansi ya IVF kupata watoto, ndipo akaanza kuchangisha.

Wapenzi hao walipatana mnamo 2012 na wakaoana Julai 2017, huku mumewe katika kila hatua akimsaidia Sarah.

Wawili hao waliamua kuunda ukurasa kwenye mitandao kwa jina GoFoundMe kuchangisha pesa ili kuwezesha ndoto yao ya kuwa wazazi.