Kimataifa

Mwanaume ahukumiwa kifo kwa ‘kumkosoa’ rais kwenye Facebook

Na REUTERS, WINNIE ONYANDO October 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANAUME mmoja raia wa Tunisia amehukumiwa kifo kwa tuhuma za kumtusi rais na kushambulia usalama wa taifa kupitia chapisho kwenye mitandao ya kijamii.

Hukumu kama hiyo haijawahi kutokea nchini Tunisia, ambapo vikwazo vya uhuru wa kujieleza vimeimarishwa tangu Rais Kais Saied achukue uongozi mnamo 2021.

Kulingana na wakili wake, Oussama Bouthalja, mwathiriwa huyo, Saber Chouchane, mwenye umri wa miaka 56, alikamatwa mwaka jana kutokana na chapisho hilo.

“Jaji katika mahakama ya Nabeul alimhukumu kifo mwanamume huyo kutokana na machapisho ya Facebook. Ni uamuzi wa kushangaza na ambao haujawahi kushuhudiwa,” Bouthalja alisema.

Ingawa mahakama mara kwa mara zimetoa hukumu za kifo nchini Tunisia, hakuna hata moja ambayo imetekelezwa kwa zaidi ya miongo mitatu.

“Hatuwezi kuamini,” Jamal Chouchane, kakake Saber, aliambia Reuters kwa njia ya simu. “Sisi ni familia inayoteseka kutokana na umaskini, na sasa dhuluma na ukosefu wa haki pia inatunyima uhuru.”

Hukumu hiyo mara moja ilizua wimbi la ukosoaji na kejeli kwenye mitandao ya kijamii miongoni mwa wanaharakati na watu wa tabaka la chini nchini humo.