Mzozo wa Iran na Amerika hautaathiri Kenya, ubalozi wa Iran wasema
Na CHARLES WASONGA
IRAN na Kenya zitaendelea kudumisha uhusiano wa kirafiki licha ya Kenya kuendelea kuwa mshirika wa Amerika inayozozana na taifa hilo la ghuba ya Uajemi.
Katibu anayesimamia masuala ya kisiasa katika ubalozi huo Tohid Afzali Jumatano alisema Kenya na Iran zimejitolea kuendelea kudumisha ushirikiano kati yao ambao umenawiri kwa miaka mingi.
“Ningetaka kutoa ujumbe kwa Wakenya wote kwamba, nyingi ni marafiki zetu. Mzozo kati yetu na Amerika hautaendelezwa hadi Kenya ingawa Amerika ina uhusiano na Kenya katika nyanja mbalimbali,” akasema.
“Tuko hapa kuimarisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na Kenya, na uhusiano huo hautaathiriwa kwa njia yoyote na mzozo unaoendelea kati yetu na Amerika,” Bw Afzali akakariri.
Afisa huyo wa ubalozi wa Iran aliwashukuru Wakenya kwa kutuma jumbe nyingi za rambirambi kwa Iran kufuatia kuuawa kwa Luteni Jenerali Qasem Soleimani mnamo Januari 2, 2020. Kiongozi huyo wa kikosi cha Iran kwa jina Quds Force aliuawa katika shambulio lililotekelezwa na droni ya Amerika nchini Iraq.
Mnamo Januari 4, 2020, Makamu wa Rais wa Amerika Mike Pence alidai kuwa Jenerali Qasem ndiye alihusika na mashambulio ya kigaidi nchini Kenya mnamo mwaka 2011.
“Aliamuru kikosi chake kupanga mashambulio ya mabomu dhidi ya raia wasio na hatia nchini Uturuki na Kenya mnamo 2011,” Pence akasema kupitia ujumbe wa Twitter.
Akijibu kuhusu madai hayo, Bw Afzali alihoji sababu ya Amerika kuingiza Kenya katika uhasama kati ya mataifa hayo mawili.
“Kuna tofauti kati ya serikali ya Iran na raia. Hatuwezi kuwaua raia,” Afzali akasema.
Pia akauliza: “Mbona wanahusisha serikali ya Kenya na mzozo baina ya Iran na Amerika?”