Kimataifa

Ngono ni muhimu sana katika maisha ya uzeeni, aeleza ajuza

January 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA Na PETER MBURU

AJUZA mmoja wa miaka 83 ameibuka mtu wa kuzungumziwa sana mitandaoni, baada ya kuanzisha mtandao wa midahalo ya masuala ya ngono.

Bi Joyce Williams wa kutoka Yorkshire anasema kuwa anaamini kuwa ngono inafaa sana uzeeni, akipendekeza kutumiwa kwa vifaa vya kujiridhisha kimwili (sex toys) kwa wazee wa zaidi ya miaka 80.

Katika chapisho moja mitandaoni, ajuza huyo alisema “vifaa vya kujiridhisha kingono vinafaa kwa watu wakongwe.”

“Ngono katika miaka ya uzeeni inasisimua mwili na kuusaidia. Tuna wakati wa kutosha kujiburudisha na ni vyema kuwa na mbinu tofauti za kufanya hivyo,” akasema.

Mama huyo aidha mbeleni amekiri kuwa watengenezaji wa vifaa hivyo vya ngono wamepokea manunuzi mengi ya vifaa hivyo kutoka kwa wazee, japo akisema kuwa wakongwe wengi wanaaibika kuvinunua madukani.

Alianzisha blogi yake ya kuzungumzia masuala hayo, kwa jina Grandma Williams, alipokuwa na miaka 81, kwa lengo la kuonyesha kuwa ngono si kitu cha vijana pekee.

Cha kushangaza ni kuwa anaungwa mkono katika juhudi zake na mwanaye wa kiume, Andrew na mjukuu wake Sam. Mumewe wa pili David ambaye ana miaka 81 pia anamuunga mkono.

Tangu miaka yake ya ujanani, alisema kuwa amekuwa na mapenzi ya kuanzisha blogi ya kufunza watu kuhusu masuala ya ngono na mahaba.

“Ni hicho tu nilichohitaji kuelezwa kuwa nilihitaji kukifanya. Kumekuwa na mafunzo mengi n ahata magazeti ya kuelimisha vijana kuhusu mahaba, lakini je, nani anayefunza kuhusu mahaba kwa wazee. Kwanini ikubalike vijana kuzungumzia kuhusu masuala yao wazi nao wazee kuzimwa?” akauliza.

Alieleza kuwa kumekuwa na dhana kuwa wazee wanapofikisha miaka 70 na kuendelea hawafanyi ngono tena, japo akisema hiyo si kweli “na wazee pia hawazungumzii hili.”

Alipofungua blogi yake, kwa wakati mfupi alipokea maelfu ya wafuasi, wakizidi 2,500. Mwaka uliopita, aliteuliwa katika mashindano ya kuzawadi mabloga nchini Uingereza.

“Na kuna njia mpya ya wazee kujiburudisha kimahaba hata wakiwa wakongwe- tuna muda wa kujiburudisha.”

Alieleza kuwa hata wakati mwingine, wakongwe wanalazimika kujifanya wagonjwa ili waweze kusisimuliwa kimahaba na watu wanaokuja kuwashughulikia.

Mbali na mafunzo ya mahaba kwa wakongwe, Joyce aidha anatoa mafunzo ya jinsi ya watu kukubali mabadiliko wanapozeeka.

“Ngono ni kipengee tu cha ujumbe wangu na kurekebisha dhana waliyo nayo watu dhidi yetu wazee,” akamaliza.