• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Obama amshutumu Trump kwa kuhujumu demokrasia

Obama amshutumu Trump kwa kuhujumu demokrasia

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

RAIS mstaafu wa Amerika Barack Obama amemshtumu vikali Rais Donald Trump kwa kukataa kukubali kushindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 3.

Katika mahojiano na runinga ya NPR ya nchini Amerika, Jumatatu, Obama alisema kuwa hatua ya Rais Trump kukataa matokeo ya uchaguzi ni moja tu ya mifano ambapo kiongozi huyo amekiuka misingi ya demokrasia wakati wa uongozi wake.

Rais mstaafu alitoa kauli hiyo huku Rais Trump akishikilia alishinda uchaguzi na ameenda kortini kusaka haki.

Rais Trump amezuia kamati maalum iliyoundwa kuandaa mipango ya kuapisha Rais Mteule Joe Biden na makamu wake Kamala Harris, kutumia fedha za umma.

“Serikali ya Trump imepoteza muda mwingi wa kufanya maandalizi ya kumwapisha Biden. Hatua hiyo itaathiri raia wa Amerika na ulimwengu mzima. Nchi hii kwa sasa inakabiliwa na janga la virusi vya corona na kudorora kwa uchumi na masuala hayo yanahitaji kushughulikiwa kwa dharura,” akasema Obama.

Obama alisema kuwa tabia hiyo ya Trump ni tofauti na alivyomfanyia alipompokeza uongozi wa Amerika miaka minne iliyopita.

Alisema Rais Mstaafu George W Bush wa Republican alimkabidhi mamlaka kwa amani Obama alipochukua hatamu za uongozi mnamo 2008.

“Kulikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa baina yangu na George W Bush, lakini niliposhinda urais alinipokeza mamlaka bila kunihangaisha.

“Serikali ya Bush ilinifahamisha hali halisi kuhusiana na masuala mbalimbali, ikiwemo hali ya uchumi na vita katika mataifa ya Afghanistan na Iraq,” akasema Obama.

Rais Mteule Biden na Harris wa chama cha Democratic wanatarajiwa kuapishwa Januari 20, 2021, baada ya kumbwaga Trump wa Republican.

Mtaalamu wa maradhi ya kuambukizwa, Dkt Anthony Fauci, Jumatatu alisema kuwa kuna haja ya wataalamu wa afya kuanza kushirikiana na kamati ya washauri walioteuliwa na Rais Mteule Biden kukabiliana na janga la virusi vya corona hata kabla ya kuapishwa.

Wanasiasa wa Repblican wameunga mkono hatua ya Rais Trump kukataa kukubali matokeo hadi pale haki itakapopatikana mahakamani.

Lakini wapinzani wake wa chama cha Democratic wamemshutumu vikali Trump kwa kuhangaisha Biden ambaye ni mshindi halali wa uchaguzi uliopita.

Obama jana alisema kuwa Biden atalazimika kufanya kazi na baadhi ya maseneta wa Republican baada ya chama cha Democratic kushindwa kupata maseneta 51 waliotakiwa ili kudhibiti Seneti.

Obama leo Jumanne anatarajiwa kuzindua kitabu chake chenye kichwa: ‘A Promised Land’.

You can share this post!

Kibwana anuia kusaka urais kwa tiketi ya KLM

BURUDANI: DJ aeleza jinsi Covid-19 ilivyoyumbisha mikataba,...