Papa ataka wahamiaji waheshimiwe na vita vikome
VATICAN CITY
PAPA Leo XIV amesema kuwa wahamiaji lazima waheshimiwe na akatoa wito kwa mataifa yasitishe utengenezaji wa silaha hatari za kivita.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni alitoa wito wa amani na maridhiano kati ya mataifa mbalimbali. Alikuwa akizungumza Vatican wakati wa mkutano wake wa kwanza na wanadiplomasia kutoka Ulimwengu tangu achaguliwe wiki jana.
Papa ambaye anatoka Amerika na aliishi miaka mingi Peru, alijirejelea kama mwenye asili ya wahamiaji. Alitoa wito wa huruma na hekima katika kuwashughulikia wahamiaji au waliotoka nchi zao kutokana na sababu mbalimbali kisha kuhamia mataifa mengine.
Katika hotuba yake, Papa Leo pia alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki linathamini ndoa na linatambua tu ndoa kati ya mwanamume na mwanamke wala si ile ya jinsia moja. Alirejelea familia kama asasi na kiini cha amani katika jamii.
Hotuba yake ilijikita katika kwenye amani, haki, uhuru wa kuabudu na kiini cha uhasama katika ulimwengu pamoja na kazi za kidiplomasia. Alisema baada ya kuishia Amerika Kusini na Kaskazini pamoja na kuzuru mataifa mbalimbali, anafahamu tamaduni na mahitaji ya raia wengi.
Pia alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki linapinga uavyaji mimba kisha akataja Ukanda wa Mashariki ya Kati na Ukraine kama maeneo ambayo raia wanateseka sana kutokana na ukosefu wa amani.