PAPA LEO XIV aombea TZ na kuhimiza amani Sudan
PAPA Leo XIV ameiombea Tanzania kufuata wimbi la machafuko lililogubika nchi hiyo kutokana na uchaguzi wa urais na ubunge uliofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni alitumia sala yake ya Jumapili, Novemba 2, 2025 katika uwanja wa Kanisa la St Peter’s kuhimiza amani na kukomeshwa kwa fujo katika miji mbalimbali nchini humo.
“Hebu pia tuombee Tanzania, ambako makabiliano yalitokea, na kuacha watu kadhaa wakiwa wamejeruhiwa. Nahimiza kila mmoja kujiepesha na aina zozote za fujo na kufuata mkondo wa mazungumzo,” Papa Leo akasema katika mahubiri yake kwa maelfu ya waumini na wafuasi.
Watu kadhaa wanahofiwa kufa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya ghasia kutokea wakati wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Serikali ya Tanzania, hata hivyo, haijatoa takwimu rasmi ya wale waliokufa na wale ambao walijeruhiwa.
Wakati huo huo, shirika la Habari la Vatican News limeripoti kwamba Papa Leo XIV amehimiza uwepo wa amani katika nchi ya Sudan inayozongwa na vita.
Amekashifu mashambulio na ukatili dhidi ya raia na kuhimiza kuondolewa kwa vizuizi vinavyozuia kupitishwa kwa misaada ya kibinadamu kwa wahanga wa vita hivyo.
Vita hivyo, vililipuka mnamo Aprili 2023 kati ya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) na Jeshi la Ulinzi la Sudan (SAF).
Jumla ya watu milioni 4 wametoroka makwao kutokana vita hivyo katika miji mbalimbali.
Aidha, Sudan, yenye jumla ya watu milioni 51, inakumbwa na kero la baa la njaa na milipuko ya kipindupindu na magonjwa mengine.