Polisi lawamani kwa mauaji ya waandamanaji Jumanne
Na AFP
ABUJA, Nigeria
VIKOSI vya usalama nchini Nigeria vimedaiwa kuwaua waandamanaji kadhaa mnamo Jumanne, yalisema mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Polisi wanadaiwa kuwafyatulia risasi watu waliokuwa wakiandamana katika sehemu moja jijini Lagos kwa kukiuka muda uliowekwa watu kutotoka nje.
Kufikia Jumanne, watu 18 walikuwa wameripotiwa kuuawa kwenye makabiliano kati ya polisi na waandamanaji hao.
“Vikosi vya usalama viliwaua watu waliokuwa katika eneo la Lekki, mjini Lagos,” alisema Isa Sanusi, ambaye ndiye msemaji wa shirika la Amnesty International nchini humo.
Eneo hilo limekuwa miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa ngome kuu ya maandamano hayo.
Msemaji alieleza mashirika hayo yanafanya kila juhudi kubaini idadi kamili ya watu waliouawa.
Waandamanaji wamekuwa wakilalamikia ukatili wa Kikosi Maalum cha Kukabiliana na Uhalifu (SARS) wakisema kimekuwa kikiwaua watu ovyo bila kubaini ikiwa ni wahalifu.
Serikali imekuwa ikitumia kikosi hicho, ambacho kinajumuisha polisi kukabili ongezeko la visa vya uhalifu.
Walioshuhudia walisema polisi walifyatua risasi kwa umati wa zaidi ya watu 1,000 waliokuwa wakifanya maandamano ya amani.
“Sote tulikuwa tumeketi chini bila usumbufu wowote. Walizima taa za barabarani ambapo kila mmoja alianza kupiga kamsa,” akasema mwandamanaji, aliyetambuliwa kama Toye.
“Walikuja tulikokuwa. Hatukujua walikuwa watu gani. Walikuwa wakifyatua risasi ovyo huku kila mmoja akikimbilia usalama wake katika sehemu tofauti,” akasema mwandamanaji mwingine, aliyetambuliwa kama Innocent.
“Kwa sasa, kuna watu wawili ambao nimelazimika kuwapeleka hospitalini wakiwa katika hali mahututi. Mmoja alipigwa risasi kwenye mgongo huku mwenzake akiwa na jeraha la risasi tumboni mwake,” akasema.
Mtumbuizaji mmoja maarufu alipeperusha video ya moja kwa moja iliyoonyesha watu wakimtoa mwenzao risasi kutoka mwilini mwake.
Awali, waandamanaji katika eneo hilo waliimba wimbo wa kitaifa huku wakiapa kubaki barabarani licha ya maagizo kuwataka kwenda nyumbani.
Maandamano dhidi ya kikosi hicho yalianza wiki mbili zilizopita, watu wengi wakieleza kukasirishwa na utendakazi wake.
Hapo Jumanne, gavana wa jimbo la Lagos, Babajide Sanwo-Olu aliagiza kufungwa kwa maeneo yote ambayo yanatumika na waandamanaji kama ngome yao.
Alisema maandamano hayo “yamegeuka kuwa tishio kuu la kwa uchumi na usalama wa taifa hilo” baada ya ghasia kuripotiwa katika baadhi ya maeneo.
“Wahalifu sasa wanatumia kisingizio cha maandamano kuendeleza uhalifu,” akasema kwenye Twitter, akisisitiza kuwa ni watu wanaotoa huduma muhimu pekee ambao wataruhusiwa kuwa kwenye jiji hilo.
“Hatutaruhusu ukiukaji wa sheria kuendelea katika jimbo letu,” akaeleza.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakiwalaumu wahalifu “waliofadhiliwa” kwa kuwashambulia waandamanaji.