• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 11:48 AM
Polisi nchini Nigeria waanza operesheni ya kuwasaka wahalifu

Polisi nchini Nigeria waanza operesheni ya kuwasaka wahalifu

Na MASHIRIKA

LAGOS, NIGERIA

POLISI wa Nigeria wamesema wameanza msako wa kupambana na wahalifu kote nchini humo ili kuimarisha usalama.

Hii ni baada ya machafuko kukithiri nchini humo kwa wiki moja ambapo zaidi ya watu 70 waliuawa na mali ya thamani kubwa kuharibiwa.

Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, msemaji wa Polisi Frank Mba alisema serikali imeamuru polisi kuanzisha operesheni ya ya kukomesha ghasia zilizokumba miji kadha nchini Nigeria.

Mba alionya kuwa wahalifu watakabiliwa kwa mkono wa sheria.

Kwa muda wa siku saba zilizopita ghasia zimeripotiwa katika miji kadha nchini humo baada ya watu walioshukiwa kuwa wahalifu kuingilia maandamano ya amani ya raia waliokuwa wakikashifu mienendo la polisi kutumia nguvu kupita kiasi.

Shughuli za kiuchumi ziliathiriwa katika miji mikubwa nchini Nigeria huku wahuni hao walifunga barabara kuu kwa kuteketeza magurudumu, fanicha na bidhaa nyinginezo.

Rais Muhammadu Buhari alilaani vitendo hivyo Ijumaa baada ya kufanya kikao na viongozi wa zamani wa Nigeria kujadili hali ya usalama nchini humo.

“Inasikitisha kuwa maandamo yaliyonuiwa kuwa halali ambapo vijana walikwa wakilaani ukatili wa kikosi maalum cha polisi wa kukabiliana na wahalifu sugu yalitekwa na wahalifu,” Buhari akasema katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Mnamo Jumapili, Mba alisema polisi wanapanga kuziba “nafasi” zote ambazo wahalifu hutumia kunawiri.

Hata hivyo, alitoa wito kwa maafisa hao kutumia njia halali kuzuia vitendo vya uvunjaji sheria na uharibifu wa mali.

Jiji la Lagos lenye shughuli nyingi za kiuchumi, polisi waliwaambia wanahabari kwamba kufikia Jumapili washukiwa 229 wamekamatwa kwa makosa kadha. Makosa hayo ni kama vile uteketezaji mali, mauaji, wizi, uharibifu wa mali na mashambulizi ya watu.

Nchini Kenya, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alilaani ghasia hizo huku akitaka serikali ya Nigeria kuchukua hatua muafaka kuzizima.

“Kazi ya polisi ni kulinda raia na kupambana na wahalifu wala sio kuwafyatuliwa risasi na kuwaua raia wasio na silaha jinsi ilivyoshuhudiwa nchini Nigeria. Serikali ya nchi hiyo inapasa kuzuia vitendo kama hivyo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu,” akasema Bw Odinga ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa Muungano wa Afrika (AU) kuhusu miundomsingi.

You can share this post!

Hamilton ampiku Schumacher kwenye mbio za magari ya...

Waziri wa Viwanda ahusika kwenye ajali