Kimataifa

Polisi Tanzania waanza kuchunguza madai ya kutekwa kwa mwanasiasa Polepole

Na MASHIRIKA, WINNIE ONYANDO October 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JESHI la Polisi nchini Tanzania limeanza kuchunguza taarifa za kutekwa nyara kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na mwanasiasa Humphrey Polepole.

Saa chache baada ya taarifa za kutekwa kwake kusambaa mitandaoni, jeshi lilisema kuwa tayari limeanza kufanya uchunguzi wa madai ya kutekwa kwake au kutoweka kwake.

Jeshi hilo lilisema, awali walikuwa wakimtafuta Polepole ili aweze kuwasaidia kuhusiana na tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa na limesisitiza kuwa wanafanyia uchunguzi taarifa za kutekwa kwake.

Jumanne asubuhi, taarifa za kutoweka kwa Polepole zilisambaa kupitia mitandao ya kijamii huku zikionyesha nyumba inayodaiwa kuwa ni makazi yake, ikiwa imeharibiwa na damu kuonekana sakafuni.