Raila kusafiri Afrika Kusini kupatanisha Machar na Kiir
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anaondoka nchini Alhamisi asubuhi kwenda Afrika Kusini ambako anatarajiwa kukutana na kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini Riek Machar katika juhudi za kurejesha amani nchini humo.
Bw Odinga pia anatarajiwa kukutana na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye anatarajiwa kupiga jeki juhudi za kupatanisha Dkt Machar na Rais Salva Kiir.
Duru ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Odinga kwanza atakutana na Rais Ramaphosa kabla ya kufanya kikao na Dkt Machar ambaye amekuwa akizuiliwa ndani ya nyumba moja kitongojini mwa Johannesburg kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Wengine walioko katika ujumbe wa Bw Odinga ni pamoja na wakili wake, Paul Mwangi, aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Amerika Elkana Odembo na Kiranja wa upinzani katika bunge la kitaifa Junet Mohammed.
Kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi Jumatano alisema ziara ya Bw Odinga nchini Afrika Kusini inapiga jeki sifa yake kama kiongozi mwenye hadhi ya juu barani Afrika.
“Wachache wetu hawajatambua hadhi ya Bw Odinga. Heshima anayopewa katika bara la Afrika na maeneo mengine ulimwenguni ni ya juu mno,” akasema Bw Mbadi akitoa mfano wa mchango wa Bw Odinga katika mchakato wa upatanishi nchini Ivory Coast mnamo 2010.
Mkutano kati ya kiongozi huyo wa upinzani na Dkt Machar unajiri siku chache baada yake kufanya mazungumzo na Rais Kiir kwa saa saba jijini Juba ambapo walijadili mzozo uliotokea nchini humo tangu Desemba, 2013.