Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza afariki
NA MASHIRIKA
RAIS wa Burundi Pierre Nkurunziza amefariki Jumanne jioni kutokana na msukumo wa moyo akiwa na umri wa miaka 55, serikali ya nchi hiyo imetangaza.
Bw Nkurunziza, ambaye ni wa kabila la Hutu alikuwa kiongozi wa mapigano ya kuondoa serikali mamlakani na aliapishwa kuwa rais wa pili wa nchi hiyo kupitia uchaguzi wa kitaifa hapo 2005 baada ya mapigano hayo kusitishwa.
Hapo Machi 2018, chama tawala cha CNDD-FDD kilimtawaza Bw Nkurunziza kama ‘kiongozi wa milele mwenye mamlaka makuu.’
Mkewe mwendazake Bi Denise Bucumi Nkurunziza alisafirishwa hadi jijini Nairobi siku 10 zilizopita kwa matibabu baada ya kuugua Covid-19.
Duru kutoka Hospitali ya Aga Khan, Nairobi zimesema kuwa Bi Nkurunziza anaendelea kupokea matibabu ya ugonjwa mwingine ambao amekuwa akiugua.
Siku moja iliyopita, ripoti iliibuka kuwa Bw Nkurunziza alikuwa amepatikana na virusi vya corona na kukimbizwa hospitalini.
Mwezi uliopita, chama tawala cha nchi hiyo kilishinda uchaguzi wa urais kupitia mwaniaji wake Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye, aliyezoa asilimia 68 ya kura zilizopigwa.
Uchaguzi huo ulitia kikomo utawala wa Bw Nkurunziza wa miaka 15 baada ya jaribio lake la kuwania urais kwa mara ya tatu kuzua machafuko na maandamano ya kisiasa.