Kimataifa

Rwanda taabani kwa kuita waziri wa Afrika Kusini 'malaya'

December 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

RWANDA imejipata matatani baada ya mtandao unaoounga mkono serikali kumrejelea waziri mmoja wa wa Afrika Kusini kama ‘malaya’.

Serikali ya Afrika Kusini Jumanne ilimwalika balozi wa Rwanda nchini humo kutoa ufafanuzi kuhusiana na kauli hiyo iliyotolewa na tovuti hiyo inayounga utawala wa Rais Paul Kagame.

Tovuti hiyo ilimtaja Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini, Lindiwe Sisulu, kama ‘kahaba’.

Mbali na tovuti hiyo, inadaiwa kuwa afisa mkuu katika serikali ya Rais Kagame pia anaendelea kumshambulia Bi Sisulu kupitia mtandao wa Twitter.

Uhasama baina ya mataifa hayo mawili ulianza pale Bi Sisulu alipokutana na mkosoaji mkuu wa kiongozi wa Rwanda Rais Kagame ambaye sasa anaishi mafichoni nchini Afrika Kusini.

Sisulu, wiki iliyopita, aliambia wanahabari jijini Johannesburg kuwa alikutana na kiongozi huyo wa upinzani Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa ambaye ni mkuu wa majeshi wa zamani wa Rwanda.

Waziri huyo alisema kuwa Nyamwasa ambaye tayari amebuni chama cha upinzani yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais Kagame.

Nyamwasa amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu 2010 baada ya kutofautiana vikali na Rais Kagame.

Waziri msaidizi wa masuala ya kigeni wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alishutumu mkutano huo baina ya Sisulu na Nyamwasa.

Nduhungirehe alimtaja Nyamwasa kama mhalifu na jambazi.

“Ikiwa Afrika Kusini inataka kuzungumza na jambazi basi iko huru kufanya hivyo bila kuhusisha Rwanda. Hatuna wakati na mhalifu,” akasema Nduhungirehe.

Katika kichwa cha habari, tovuti hiyo ya serikali ilimrejelea Sisulu kama ‘kahaba’ wa Nyamwasa, kulingana na serikali ya Afrika Kusini.

Habari hiyo baadaye iliondolewa kwenye tovuti hiyo lakini tayari ilikuwa imenakiliwa na tovuti nyinginezo pamoja na wanablogu.

Msemaji wa Sisulu, Ndivhuwo Mabaya, alisema kuwa balozi wa Rwanda nchini Sudan Kusini alihojiwa mara kadhaa kutokana na kauli hiyo.

Wakati huo huo, balozi wa Afrika Kusini nchini Rwanda ameagizwa kurejea nyumbani kwa mashauriano.

Mnamo 2014, Afrika Kusini iliwatimua maafisa watatu kutoka ubalozi wa Rwanda nchini humo baada ya watu wasiojulikana kushambulia makazi ya Nyamwasa jijini Johannesburg. Rwanda ililipiza kisasi kwa kuwafukuza maafisa sita wa Afrika Kusini jijini Kigali.

Nyamwasa amenusurika majaribio mawili ya kumuua huku akiwa uhamishoni Afrika Kusini.

Mahakama ya Afrika Kusini, mnamo 2014, iliwapata watu wanne na hatia ya kummiminia risasi tumboni Nyamwasa ambaye baadaye alitaja shambulio hilo kuwa la kisiasa.

Uhusiano baina ya Rwanda na Afrika Kusini ulitumbukia nyongo mnamo 2014 baada ya afisa mkuu wa ujasusi wa Rwanda Kanali Patrick Karegeya, kupatikana ameuawa hotelini jijini Johannesburg.