Shemejiye Trump kuzuru Kenya na Maziwa Makuu
MASSAD Boulos, mshauri mpya wa masuala ya Afrika katika Wizara ya Masuala ya Kigeni nchini Amerika atazuru Kenya wiki hii.
Bw Boulos ni babake Michael Boulos ambaye ni mumewe Bi Tiffany; bintiye Rais wa Amerika Donald Trump.
Aidha, yeye ni mshauri wa rais kuhusu masuala ya Uarabuni na Mashariki ya Kati.
Boulos ataandamana na Naibu Waziri wa Masuala ya Kigeni anayesimamia Masuala ya Afrika Corina Sanders, Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika ilisema Jumanne.
Wawili hao pia watazuru mataifa ya Maziwa Makuu, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda na Rwanda, kuanzia Aprili 4, 2025.
“Mshauri mkuu Boulos na ujumbe wake watakutana na marais na viongozi wa kibiashara kuendeleza juhudi za kuleta amani mashariki mwa DRC na kuimarisha uwekezaji kutoka sekta ya kibinafsi Amerika,” ikasema taarifa kutoka kwa msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni wa Amerika Tammy Bruce.
Wadadisi wanasema kuwa Bw Boulos aliteuliwa katika wadhifa huo mpya kutokana na hali kwamba ameishi kwa miaka mingi nchini Nigeria.
Ni shemeji wa pili wa Trump kuteuliwa na rais huyo baada ya Charles Kushner, ambaye ni baba mkwe wa bintiye rais huyo, Ivanka.
Kushner aliteuliwa kuwa balozi wa Amerika nchini Ufaransa.
Bw Boulos alichangia katika ushindi wa Trump kwani alimsaidia kuvutia kura za Waamerika-Waarabu na Waislamu.
Baadhi ya wapigaji kura walikerwa na utawala wa Joe Biden kuhusiana na vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Akitangaza uteuzi wake, kupitia mtandao wa kijamii, Bw Trump alisema Boulos alichangia pakubwa katika “kuundwa kwa miungano mipya na Waarabu ambao ni raia wa Amerika.”
Kinyume na teuzi zingine za Rais Trump, uteuzi wa Bw Boulos kama mshauri haukuhitaji kuidhinishwa na Seneti.
Utawala wa Trump unavutiwa na taifa la DRC kutokana na utajiri wa madini ulioko eneo hilo.
Baadhi ya madini yanayopatikana mashariki mwa nchi hiyo hutumika kutengeneza vifaa vya kieletroniki.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga