Kimataifa

Shinikizo jeshi liachilie mamlaka kuanza Juni 30

June 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, Sudan

VIONGOZI wa waandamanaji wametangaza kuwa wataanza maandamano tena baada ya Baraza la Kijeshi linaloongoza Sudan kukataa pendekezo la serikali ya Ethiopia la kutaka raia saba wajumuishwe katika serikali ya mpito.

Wanajeshi pamoja na viongozi wa waandamanaji wamekosa kuafikiana kuhusu muundo wa serikali ya mpito itakayoongoza Sudan baada ya kubanduliwa mamlakani kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Omar al-Bashir mnamo April 11, 2019.

Ethiopia iliwasilisha mapendekezo yake ikitaka serikali ya mpito ijumuishe wanajeshi saba, raia saba na wadhifa mmoja wa mtu asiyeegemea upande wa jeshi au raia.

Msemaji wa Baraza la Kijeshi (TMC) Luteni Jenerali Shams al-Din Kabbashi, alisema kuwa wanajeshi wako tayari kukubaliana na pendekezo la Umoja wa Afrika (AU).

“Pendekezo la AU lilikuwa la kwanza kuwasilishwa kwetu, lakini hatutajadili pendekezo la Ethiopia,” akasema Kabbashi.

Baraza la kijeshi halikuweka wazi mapendekezo yaliyotolewa na AU.

Ismail al-Tag, msemaji wa Chama cha Wasomi nchini Sudan, alisema Jumanne kuwa maandamano yataanza wiki ijayo ili kushinikiza wanajeshi kukabidhi raia mamlaka.

“Wananchi wajiandae kwa ajili ya maandamano makubwa yatakayoanza Juni 30. Tunalenga kuhakikisha kuwa wanajeshi wanakabidhi mamlaka kwa watu wa Sudan. Maandamano hayo hayatakoma hadi pale tutakabidhiwa mamlaka ya kuongoza nchi,” akasema Tag.

Maandamano sambamba na maadhimisho

Maandamano hayo pia yatakuwa maadhimisho ya miaka 30 tangu kufanyika kwa mapinduzi yaliyomwezesha Omar al-Bashir kuingia mamlakani mwaka 1989.

Msemaji wa Baraza la Kijeshi Kabbashi alisema AU na Ethiopia wanafaa kuunganisha mapendekezo yao ili yaweze kujadiliwa kwa pamoja.

“Tumewataka wapatanishi kuunganisha mapendekezo yao na kuwasilisha stakabadhi moja ili tuweze kuyajadili,” akasema Kabbashi.

Jon Temin, mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali la Freedom House, anasema jeshi limekuwa likitumia visingizo visivyo na mashiko ili kupoteza wakati na kuendelea kukatalia mamlakani.

“Huo ni ujanja wa kutaka wapatanishi wachoke na waachane na Sudan ili waendelee kuendesha serikali,” akasema.

Mazungumzo baina ya wanajeshi na viongozi wa waandamanaji yalisambaratika baada ya maafisa wa usalama kushambulia na kuua waandamanaji zaidi ya 40 waliokuwa wameketi nje ya makao makuu ya kijeshi mnamo Juni 3.

Jeshi baadaye liliomba radhi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kutawanya waandamanaji. Jaribio la mapinduzi nchini Ethiopia Jumapili pia limekuwa pigo kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuendeleza juhudi zake za kupatanisha jeshi na raia nchini Sudan.