Kimataifa

Tovuti ya ngono yazimwa, mwanamke mmiliki atupwa jela

January 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MMOJA wa waasisi wa mtandao mkubwa zaidi wa video za ngono nchini Korea Kusini amehukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani na mahakama moja ya Seoul kwa kuongoza usambazaji wa fikra chafu.

Mwanamke huyo kwa jina Song alikuwa akimiliki mtandao wa Soranet, ambao una zaidi ya watumizi milioni moja na ambao una maelfu ya video zilizoharamishwa.

Nyingi kati ya video hizo zilirekodiwa kisiri na kuwekwa mitandaoni bila idhini ya wahusika.

Kutengeneza na kusambaza video za kingono kumeharamishwa Korea kusini na mtandao huo wa Soranet ulifungwa baada ya umma kulalamika.

Miezi michache iliyopita, wanawake taifa hilo waliandaa maandamano mitaani, wakiitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanaotoa na kusambaza kwa umma video za ngono.

Bi Song aidha alitozwa faini ya Sh100 milioni na kuamrishwa kupitia saa 80 za mafunzo kuhusu jinsi ya kuzuia dhuluma za kingono.

Mwanamke huyo wa miaka 46 ni mmoja wa wamiliki wane wa mtandao huo, akiwemo mumewe, ambao wamekuwa wakiendesha biashara hiyo kati ya 1999 na 2016 wakitumia kompyuta za nje ya nchi hiyo, ripoti kutoka Korea zikasema.

Alitorokea New Zealand wakati polisi walianza kuchunguza mtandao huo 2015 lakini alilazimishwa kurejea Korea Kusini wakati pasipoti yake iliharamishwa.

Alipofika mahakamani, alikana mashtaka na kudai kuwa ni mumewe na wanandoa wengine wawili ambao walikuwa wakiendesha mtandao huo.

Hata hivyo, wamiliki wengine watatu ambao wana pasipoti za nje ya nchi hiyo bado hawajakamatwa.

Nyingi za kamera za kisiri za mtandao huo ziliwekwa chooni na vyumba vya kubadilishia nguo ama kusambazwa na wapenzi baada ya kukosana ili kulipiza kisasi.

Baadhi ya wanawake waliotokea katika video hizo waliishia kujiua.