Kimataifa

Trump akubali kuhojiwa katika uchunguzi wa FBI kuhusu jaribio la mauaji

Na MASHIRIKA July 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

PITTSBURGH, AMERIKA

RAIS wa zamani wa Amerika Donald Trump amekubali kuhojiwa katika uchunguzi unaoendeshwa na shirika la ujasusi la Amerika (FBI) kuhusu jaribio la kumuua afisa mmoja alisema huku maswali yakiendelea kuulizwa kuhusu kisa hicho.

Kevin Rojek, ambaye ni ajenti maalum anayesimamia afisi ya nyanjani ya FBI mjini Pittsburgh alisema Jumatatu kuwa shirika hilo linataka linataka “kupata kauli ya Trump kuhusu aliyoshuhudia siku hiyo”.

“Rais wa zamani ambaye ni mgombeaji wa urais wa chama cha Republican katika uchaguzi wa Novemba 5, 2024 amekubali kuhojiwa kama mwathiriwa.

“Mahojiano hayo yatakuwa sawa na yale tunayofanywa kwa waathiriwa wa visa mbalimbali tunavyochunguza,” Rojek akasema.

Hata hivyo, afisa huyo hakufichua siku ambayo mahojiano hayo yataendeshwa wala mahala patakapofanywa.

Trump, ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa FBI, alipigwa risasi sikioni wakati wa mkutano wa kampeni katika jimbo la Pennsylvania mapema mwezi huu.

Tukio hilo lililaaniwa pakubwa huku maswali yakiibuliwa kuhusu maandalizi ya kiusalama yaliyofanywa kabla ya kuanza kwa mkutano huo.

Mashahidi walisema mshukiwa, Thomas Matthew Crooks, 20, alimshambulia Trump kwa risasi baada ya kupanda kwenye paa la jukwaa la mkutano.

Mtu mmoja miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo aliuawa na wengine wawili wakajeruhiwa katika tukio hilo.

Wakiwahutubia wanahabari Jumatatu, maafisa wa FBI walisema hawajabaini lengo la shambulio hilo.

Wabunge wa Amerika wamezishinikiza vyombo vya usalama nchini humo kuelezea taratibu za usalama zilizowekwa kabla ya mkutano huo wa Trump ambapo alipigwa risasi.

Sasa FBI inasema kuwa inachunguza kitendo cha “ugaidi wa kinyumbani” na jaribio la kumuua rais huyo wa zamani na mgombeaji wa urais anayepigiwa upatu kushinda katika uchaguzi huo mkuu ujao.