Kimataifa

Trump ateua Rubio, anayeunga mkono Israel kutokomeza Hamas, kama waziri wa mashauri ya kigeni

Na MASHIRIKA November 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON, AMERIKA

RAIS Mteule wa Amerika Donald Trump anatarajiwa kumteua Seneta wa Florida Marco Rubio kama waziri wa masuala ya kigeni.

Trump aliyewania kupitia chama cha Republican, alimbwaga Makamu wa Rais Kamala Harris na kurejea kama Rais wa Amerika 47.

Ataapishwa Januari 20, 2025.

Vyombo vya habari Amerika vimearifu kuwa Trump ameamua kumpa Rubio jukumu hilo muhimu kutokana na urafiki wao wa kisiasa.

Waziri wa masuala ya kigeni humshauri Rais kuhusu sera mbalimbali za kigeni.

Hapo awali ilidaiwa kuwa Trump alikuwa akiwatathmini Richard Grenell na Robert O’Brien. Grenell alikuwa balozi wa Amerika kule Ujerumani katika muhula wa kwanza wa Trump kati ya 2016-2020.

O’Brien naye alikuwa mshauri wa Trump kuhusu masuala ya usalama. Wawili hao walikuwa bado ni wandani wa Rais Trump na baada ya kutokwa na kazi ya wizara ya masuala ya kigeni, Trump huenda akawapa majukumu mengine katika utawala wake.

Rubio, anahudumu katika Kamati ya Ujasusi kwenye Seneti na pia kamati inayohusika na masuala ya kigeni. Ni kati ya maafisa ambao wanatarajiwa kumsaidia Trump kutimiza ajenda yake kwa Amerika anapoanza kuunda utawala wake kabla ya kuchukua rasmi afisi mwakani.

Tangu ateuliwe katika Seneti mnamo 2010, Rubio amekuwa kati ya wale ambao wamekuwa wakionekana kuwa na mtazamo mmoja kuhusu sera za kigeni. Amekuwa akiunga Trump kuhusu msimamo wake unaopendekeza jinsi ambavyo Amerika inastahili kupambana na maadui wake kama China, Iran, Venezuela na Cuba.

Pia amekuwa akiunga mkono vita vya Israel katika ukanda wa Gaza akisema kuwa kundi la Hamas ndilo linastahili kulaumiwa kwa asilimia 100 kutokana na mauti ambayo yamekuwa yakitokea katika ukanda huo.

“Nataka waharibu na kuwafyeka kabisa kundi la Hamas pamoja na zana zao za kivita,” akasema Rubio kwenye mahojiano na vyombo vya habari Amerika mnamo Disemba mwaka jana.

“Hamas ni wanyama ambao walihusika na uhalifu na mauaji ya kusikitisha. Natumai mtachapisha hilo kwa sababu huo ndio msimamo wangu,” akaongeza.

Rubio alipambania tikiti ya Republican na Trump kuelekea uchaguzi wa 2016 lakini akaamunga mkono baada ya kubwagwa. Katika uchaguzi wa 2020 ambapo Trump alishindwa na Rais Joe Biden, Rubio alikuwa mshauri wake wa masuala ya kigeni.

Kuelekea kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Rubio alikuwa kati ya wale ambao walitajwa kuwa wangekuwa mgombeaji mwenza wa Trump.

Hata hivyo, hakupata nafasi hiyo japo mara nyingi aliungana na Trump kwenye hafla mbalimbali za kampeni.

Mnamo Jumatatu, Trump alimteua Elise Stefaniki ambaye ni mbunge wa Republican kutoka New York kama Balozi wa Umoja wa Mataifa (UN).

Pia alimteua Tom Homan ambaye alikuwa mkurugenzi kwenye idara ya uhamiaji kama mmoja wa washauri wakuu katika awamu ya pili ya utawala wake.